SIKU YA UKIMWI DUNIANI: WANANCHI WAASWA KUPIMA AFYA ZAO NA KUJIKINGA NA UGONJWA WA UKIMWI.
Wakazi wa mkoa wa Dar es salaam wameshauriwa kujitokeza
kupima afya zao mara kwa mara na kujiepusha na vitendo vinavyochangia
maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya mkuu wa mkoa
wa Dar es salaam leo jijini Dar es salaam Afisa habari wa mkoa huo Bi. Adrofina
Ndyeikiza amesema kuwa kuna umuhimu wa jamii kujitambua na kushiriki kikamilifu
katika kufanya tathmini ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi na namna bora
ya kujikinga.Amesema kila mwaka ifikapo tarehe 1 Desemba Tanzania huungana na
mataifa mengine kuadhimisha siku ya Ukimwi Duniani kwa kuwahusisha wadau
mbalimbali ambao wote kwa pamoja hupata nafasi ya kutathmini mikakati ya
kudhibiti Ukimwi iliyofanyika kwa muda wa mwaka mzima na kutafuta mbinu za
kuboresha harakati hizo.
Amesema maadhimisho hayo yatakayofanyika katika viwanja vya
Biafra jijini Dar es salaam umeichagua na kuipa heshima manispaa ya Kinondoni
kuandaa maadhimisho hayo
“Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi duniani mwaka huu yanabeba
ujumbe ule ule uliotolewa mwaka jana
ambapo kauli mbiu hii inaendelea mpaka mwaka 2015 na kwa mwaka huu jijini Dar es salaam yanafanyika katika
uwanja wa Biafra yakiongozwa na kauli mbiu ya Tanzania Bila Maambukizi Mapya,
Unyanyapaa na vifo vitokanavyo na Ukimwi Inawezekana”
Amesema lengo la kauli mbiu hiyo ni kuhamasisha na
kuelimisha zaidi jamii kuhusu VVU na Ukimwi na kubadilisha tabia ili kujikinga
na maambukizi ya mapya ya VVU, kuhamasisha jamii kuacha kabisa unyanyapaa,
unyanyasaji na ubaguzi kwa watu wanaoishi na VVU na ubaguzi kwa watu wanaoishi
na VVU na UKIMWI na kuboresha huduma za afya na tiba ya magonjwa nyemelezi na
dawa za kufubaza makali ya VVU (ARVs).
Bi. Ndyeikiza amesema kuwa mbali na maadhimisho hayo katika
mkoa wa Dar es salaam serikali kwa kushirikiana na Asasi zisizo za kiserikali
zilizo katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo zinaendelea kuwapatia wananchi
huduma za elimu, ushauri na upimaji wa hiari wa VVU katika maeneo mbalimbali.
Kwa upande wake mratibu wa Ukimwi wa mkoa wa Dar es salaam
kutoka Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini
(TACAIDS) Bw. Omary Chambo amesema kuwa jamii bado inahitaji elimu juu ya namna
na mikakati ya kukabiliana na virusi vya Ukimwi na hatimaye kupunguza
maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi.
Amesema takwimu za mwaka 2012 kwa mkoa wa Dar es salaam
zinaonyesha kuwa katika Manispaa ya Ilala hali ya maambukizi ni 8.3%, Temeke 6%
na Manispaa ya Kinondoni ni 6.7 na kuongeza kuwa vitendo vya unyanyapaa
miongoni mwa jamii kwa waathirika wa ugonjwa huo vinachangia watu wengi
wasijitokeze kupima kwa hiari ili kujua kama wanaishi na VVU.
“Vitendo vya unyanyapaa vimekua sababu ya kuwafanya wengi
wasijitokeze kupima kuhofia kutengwa na jamii pindi watakapogundulika kuwa
wameathirika , hivyo tunaendelea na juhudi ya kuwaelimisha wananchi kuepuka
vitendo hivyo na wajitokeze kupima afya zao kwa hiari” ameeleza Bw. Omary
No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA