MTANZANIA ANAYECHOMA MIILI YA MAREHEMU WA KIHINDI.
![]() |
Zuberi Mipiko |
SENTENSI iliyoandikwa katika lango kuu ni ‘Hindu Crematory’,
yaani ‘Tanuru la Wahindi la Kuchomea Maiti.’
Ipo katika eneo la Kijitonyama, jijini Dar es Salaam ambalo limetawaliwa na miti
mirefu, ikiwamo miembe, mipera na mingine isiyo na matunda. Upande wa kulia,
kuna nyumba mbili ndogo nyeupe.
Upande wa kushoto kuna kitu mfano wa kaburi lililosakafiwa
vyema pamoja na picha ya mtu anayeonekana kuwa na hadhi kutokana na mavazi
yake.
Mbele yake kuna majengo mawili makubwa yaliyoshabihiana
kiasi. Yameezekwa juu kwa bati, bali
nguzo nne kubwa zinazoshokilia paa hilo
ambalo kwa ndani limesheheni moshi mweusi.
Katikati ya jengo hilo, kuna
kitu cha chuma, mfano wa kitanda…na hilo ndilo
tanuru la kuchomea miili ya wafu, kama
zinavyohubiri mila na tamaduni za Wahindi.
Ndani ya mandhari hii anaishi Mzee Zuberi Mipiko, mwenye umri wa miaka 79
sasa.
Pamoja na ulinzi, lakini kazi yake kubwa ni kuchoma miili ya
wafu.
Mipiko, mwenyeji wa Kisarawe Mkoani Pwani anasema alianza
kazi katika tanuru hilo
mwaka 1976.
Katika miaka 36 aliyofanya kazi ndani ya tanuru hilo, amekwishachoma
maelfu ya miili ya wafu wa mataifa mbalimbali wakiwemo pia Watanzania wenzake.
Mzee Mipiko huwachomaje wafu?
Kwanza kabisa,
anasema baada ya mwili wa marehemu kuingia ndani ya jengo hilo, Wahindi huvunja nazi tatu katika kaburi lililo karibu kabisa
na lango kuu.
Baada ya hapo mwili huletwa katika tanuru lenyewe. Yeye (Mipiko ) hupanga kuni juu ya tanuru hilo ambalo limeundwa mithili ya kitanda cha
chuma.
“Mimi huanza kupanga kuni kabla hata mwili haujafika ili
kuokoa muda kwa sababu huwa napigiwa simu na kuambiwa kuwa leo kuna maiti
inakuja,” anasema
Kuni hupangwa kwa ustadi mkubwa. Zile za ukubwa kiasi hupangwa katika umbile la
reli. Magogo makubwa manne hupangwa kushoto, kulia magharibi na mashariki ya tanuru hilo.
“Kuni zinatakiwa ziwe nyingi kwa sababu kazi ya kuchoma
mwili si ndogo,” anasema Mipiko.
Kabla ya kuuweka
mwili katika tanuru, anasema ndugu wa marehemu huuzungusha mara nne,
kulizunguka tanuru hilo.
Baada ya hapo, Mwili wa marehemu ukiwa na sanda huwekwa
katikati ya kuni hizo, kichwa kikielekezwa magharibi.
Kabla ya uchomaji wenyewe kuanza, mila za Wahindu hasa
Baniani, hutaka kuhakikisha iwapo kweli ndugu yao amefariki.
Ndugu mmoja wa marehemu hutakiwa kuhakiki kwa kuchukua
kipande kidogo cha kuni chembamba
kilichoshika moto, kisha humchoma marehemu katika unyayo mara nne, huku
akilizunguka tanuru.
“Yaani, anachoma mara moja, kisha anazunguka, na anarudia
hivyo hivyo hadi mara nne,” anasema.
Hatua inayofuata ni
kuchukua moto kwa kutumia makoleo maalum, kisha kuuchanganya moto huo na mafuta
ya samli.
“Ninachofanya mimi hapo ni kuupaka uso wa marehemu kwa
mafuta ya samli, kabla ya zoezi jingine halijaanza,” anasema
Mzee Mipiko anasema husaidiana na ndugu za marehemu kuweka
moto na mafuta ya samli katika mwili, baada ya hapo moto huanza kuwaka na kwa
kawaida huwa ni mkali zaidi ya gesi.
Anasema mafuta ya samli pamoja mafuta ya marehemu mwenyewe
huufanya moto kuwa mkali kuliko kawaida.
Wakati moto unaendelea kuwaka kwa kasi, Mzee Mipiko hushika
mfuko uliojaa mbegu za ufuta na ndugu za marehemu hutakiwa kuzichota mkononi na
kuzirusha juu ya mwili unaoendelea kuungua.
“ Hayo ndiyo mazishi yenyewe sasa na wakati huo ndugu zake
huwa wamelizunguka tanuru,” anasema Mipiko
Anaongeza kuwa kwa kawaida mwili wa marehemu huchomwa na
kumalizika kabisa baada ya saa mbili au mbili na nusu.
Mwili unatakiwa kuungua na na kwisha kabisa, kinachotakiwa kubaki ni vipande vya mifupa, lakini wakati mwingine moto huweza kwisha kabisa na
wakati huo mwili bado haujamalizika.
Kama mwili haujamalizika kabisa, Mipiko hutumia koleo lake maalum
kutoa sehemu ya mwili iliyobaki, kuiweka pembeni, kisha kupanga kuni mpya… na
kuuchoma tena.
“Nikishaweka samli na mkaa pale, dakika tano tu, kila kitu
tayari,” anasema Mipiko akitabasamu
Anasema wakati mwingine mwili unaobaki unakuwa ni sehemu ya
tumbo, ambapo yeye hushuhudia utumbo au nyamanyama zilizoungua.
“Hii ndiyo kazi yangu, nausogeza taratibu, nauweka pembeni,
halafu naanza kuchoma upya,” anasema.
Baada ya mwili kuchomwa na kwisha, ndugu mmoja wa marehemu
huchukua chungu maalum kilichojazwa maji na kukiweka katikati ya miguu, kisha
anatakiwa kutazama magharibi akiyapa
kisogo mabaki ya mwili huo wakati huo
waombolezaji wote wageuke pia.
Anachofanya ndugu huyo wa marehemu akiwa amesimama ni
kuchukua jiwe na kukipiga chungu hicho kwa nguvu hadi kivunjike na maji
yamwagike kuelekea lilipo tanuru.
Baada ya tukio hilo yeye pamoja na umati wote wa waombolezaji
hutakiwa kuondoka bila kugeuka nyuma.
Mzee Mipiko anasema baada ya mwili kuchomwa na moto kumalizika kabisa, yeye huchukua
chuma kirefu mfano wa koleo na kuanza kuyatoa mabaki ya mwili huo ambayo kwa
kawaida ni vipande vya mifupa ya mwili
na fuvu, vilivyochanganyika na majivu na mkaa kutoka tanuruni.
“Nikishasogeza mabaki yaliyochanganyika na majivu na mkaa
kwa kutumia fimbo hii (anaionyesha), naanza kuvitenga vipande vya mifupa peke
yake,” anasema
Mifupa hiyo huwekwa katika mifuko maalum na hatua ya mwisho
ni ndugu kwenda kuyatupa baharini.
Mzee huyu anasema kwa miaka 36 aliyoifanya kazi hiyo ameona
na kuchoma miili mingi, hivyo amekuwa mzoefu na mahiri pengine zaidi hata ya
Wahindi wenyewe.
Anasema si raia wa India pekee ambao wanachoma wafu, bali aliwahi kuchomwa mwanamke wa
Kichagga ambaye alikuwa ameolewa na Baniani.
“Hata Wazungu wanachomwa hapa, na baadhi ya Waafrika ambao
wana imani za Kibaniani,” anasema Mzee Mipiko
Hilo
ndilo tanuru na kibarua ambacho Mipiko amekiishi kwa miaka 36 na kufanikiwa
kujipatia kipato.
Uongozi wa Hindu Mandal umemjengea nyumba yeye na familia
yake.
Anasema hana hofu juu ya kazi yake hiyo ambayo pengine yeye
ndiye mtanzania pekee anayeifanya.
“Mimi najihisi kama ni
malaika siogopi na ninazunguka katika matanuru haya wakati wote bila woga,
kwani hata mimi si nitakufa tu,” anasema
Anasema hana woga wala wasiwasi kuhusu kazi yake hiyo na
anawafundisha watoto wake wa kiume ili siku atakayoondoka duniani, basi wawe
warithi wake.
Tukutane wiki ijayo ili kufahamu ni kwa nini Wahindi huzika
wafu kwa njia hii.
Source:Mwananchi
No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA