UGAWAJI ARDHI KWA WAGENI KIHOLELA UTALIANGAMIZA TAIFA.
![]() |
| Halima Mdee - Mbunge |
MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee jana aliwasilisha hoja binafsi
bungeni, akitaka Serikali isitishe ugawaji wa ardhi kwa wageni hadi hapo
itakapokuwa imefanya tathmini na kujiridhisha kwamba wananchi watakuwa na ardhi
ya kutosha kwa kilimo cha mazao ya chakula na matumizi mengine ya kuendeleza
shughuli za maendeleo.
Mbunge huyo ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Ardhi
na Maendeleo ya Makazi, pamoja na kuituhumu Serikali kwa kuwakumbatia
wawekezaji ambao alisema wanapora ardhi ya wananchi, alisema ugawaji huo holela
wa ardhi kwa wageni usipositishwa haraka ardhi yote nzuri itachukuliwa na
wageni.
Tunampongeza mbunge huyo kwa kupeleka hoja hiyo muhimu
bungeni, hasa tukiangalia umuhimu wa suala la ardhi siyo tu katika muktadha wa
amani na utulivu katika nchi yetu, bali pia katika ustawi na maendeleo ya
wananchi ambao asilimia kubwa inategemea ardhi kwa ajili ya kilimo. Lakini pia
tunawapongeza wabunge wote waliochangia hoja hiyo kwa kuzingatia maslahi ya
taifa bila kuendekeza mitazamo ya kisiasa na kiitikadi.
Ni bahati mbaya kwamba suala la ardhi limekuwa
likitazamwa kisiasa tangu Serikali ya
Awamu ya Kwanza ilipoondoka madarakani. Kama ilivyokuwa kwa Azimio la Arusha
ambalo lilipigwa teke mara baada ya awamu hiyo kukabidhi Serikali kwa awamu
nyingine, viongozi waliokabidhiwa madaraka walifuta misingi muhimu iliyokuwa
ikisimamia suala la ardhi ambalo Azimio la Arusha lilikuwa limelipa umuhimu wa
pekee kwa lengo la kulinda umoja na amani ya nchi yetu.
Waasisi wa Azimio hilo waliangalia mbele na kugundua kwamba
suala la ardhi ni suala la kufa na kupona. Nchi yetu haiwezi kuwa na amani ya
kudumu kama wananchi wake watakosa ardhi ya kuwawezesha kuendesha maisha yao
kwa njia ya kilimo au ufugaji. Hii ni kwa sababu kilimo ndiyo uti wa mgongo wa
asilimia zaidi ya 80 ya wananchi ambao wanaishi vijijini.
Hivyo tunakubaliana kabisa na mtoa hoja kwamba kuna umuhimu
mkubwa wa kufanya tathmini ili kubaini raia wa kigeni na wa ndani waliochukua
ardhi kinyemela. Siyo siri kwamba ukwapuaji huo wa ardhi umefanyika kutokana na
viongozi wengi wa Serikali za Vijiji kupokea rushwa kutoka kwa wageni hao,
kinyume cha Sheria ya Ardhi Namba 5 ya mwaka 1999.
Miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia utitiri wa watu hao
wakiwarubuni viongozi hao wa vijiji na kufanikiwa kutwaa sehemu kubwa za ardhi
kwa bei ya kutupwa, huku wakiwaacha wananchi hao katika umaskini wa kutisha.
Nani asiyejua kwamba wengi wa watu hao wanaojiita wawekezaji wameshindwa
kuendeleza ardhi waliyoitwaa hadi leo? Pia nani asiyejua kwamba baadhi yao,
pamoja na kuchukua ardhi kubwa kwa bei ndogo, waliuza ardhi hiyo kinyemela kwa
bei ya kutisha hata bila kulipa kodi ya Serikali?
Tunakubaliana na mtoa hoja kwamba tatizo hilo kwa kiasi
kikubwa limesababishwa na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi kutokana na
kutokudhibiti hali hiyo kwa kufanya tathmini ili kupata takwimu kwa lengo la
kujua ukubwa wa tatizo. Kutofanya hivyo kumesababisha migogoro ya ardhi
isiyokwisha katika kila pembe ya nchi yetu na kuwaacha baadhi ya wananchi
wakiwa kama wakimbizi katika nchi yao.
Kama tulivyosema hapo juu, Serikali nayo imekuwa sehemu ya
tatizo kwa kuchukua ardhi ya wananchi na kuwapa wawekezaji pasipo kwanza kulipa
fidia. Wilaya zilizoathirika ni nyingi.
Moja ya wilaya ambazo wananchi wake wameathirika ni
Bagamoyo, ambapo Serikali ilitwaa kwa nguvu ardhi ya wakazi wa Kijiji cha Zinga
miaka minne iliyopita kwa kisingizio cha kutenga eneo la wawekezaji cha EPZ na
mpaka leo imeshindwa kuwalipa fidia.
Hapo ndipo mahali pa kuanzia. Haiwezekani Serikali ile njama
na wawekezaji kupora ardhi ya wananchi pasipo kuwalipa fidia kwa kisingizio cha
kukaribisha wawekezaji. Hali hiyo itakaribisha ghasia na vurugu.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA