RUFAA YA LEMA KUUNGURUMA LEO JIJINI DAR ES SALAAM.
RUFAA ya aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema),
Godbless Lema inatarajiwa kuanza kusikilizwa leo na jopo la majaji watatu wa
Mahakama ya Rufani; Salum Massati, Nathalia Kimaro na Bernard Luanda.
Pamoja na mambo mengine, rufani hiyo itakayosikilizwa Dar es Salaam, itawakutanisha wanasheria wawili ndugu; Tundu
Lissu na Alute Mghway wa upande wa mashtaka na utetezi.
Lissu ambaye ni kada wa Chadema na Mnadhimu Mkuu wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema jana kwamba atakuwapo mahakamani leo na
wakili mwenzake, Method Kimomogolo wakishirikiana kumtetea mteja wao.
Wakati Lissu akimtetea Lema, Mghway ni wakili anayewatetea
warufani wa (wajiburufaa) ambao ni makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mussa
Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel.
Makada hao walimfungulia Lema kesi katika Mahakama Kuu Kanda
ya Arusha, wakipinga matokeo yaliyompa ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2010. Hukumu ya kesi hiyo ndiyo
iliyomvua ubunge Aprili 5, 2012 mwaka huu.
Baadaye Lema alikata rufaa kupinga hukumu iliyomvua ubunge,
lakini ilitupiliwa mbali baada ya Mahakama kuridhika kuwa kulikuwa na dosari za
kisheria, kutokana na pingamizi
lililowekwa na warufaniwa.
Hata hivyo, tofauti na hoja za wakili wa warufaniwa, Mghway
kuwa kutokana na dosari hiyo, mrufani hana nafasi ya kufanya marekebisho,
mahakama ilimpa Lema nafasi nyingine ya kufungua upya rufaa hiyo baada ya
kusema dosari hizo zinarekebishika.
Mahakama hiyo ilimpa Lema siku 14 kufanya marekebisho na
kufungua tena rufaa hiyo, kazi ambayo aliitekeleza.
Awali, rufaa hiyo ilikuwa ikisikilizwa na jopo lililoongozwa
na Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman akisaidiana na Jaji Salum Massati na Jaji
Nathalia Kimaro, lakini sasa Jaji Mkuu, Othman hayuko katika jopo hilo na nafasi yake imechukuliwa na Jaji Luanda.
Katika rufaa yake ya awali, Lema alitoa hoja 18 za kupinga
hukumu ya Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha iliyomvua ubunge, lakini tarehe ambayo rufaa hiyo ilitarajiwa
kuanza kusikilizwa, wakili wa wajiburufaa, Mughwai aliweka pingamizi la awali.
Wajiburufaa katika pingamizi lao walitoa hoja tatu za
pingamizi wakidai kuwa kuna mkanganyiko
katika vifungu vya sheria kati ya vile vilivyotumika kwenye hukumu na vile vilivyokuwapo kwenye muhtasari wa
hukumu.
Hoja nyingine walidai kuwa muhtasari wa hukumu haukuwa na
mhuri wa Jaji aliyeitoa wala tarehe na hoja ya tatu ilikuwa ni utaratibu wa
kuandika muhtasari huo, kwa kutokuandika maneno; “Imetolewa kwa mkono wangu na
mhuri wa Mahakama.”
Kutokana na hoja hizo, Wakili Mghwai aliiomba Mahakama hiyo
iitupilie mbali rufaa hiyo, akidai kuwa kwa dosari hizo, mrufani hana nafasi
tena ya kuzifanyia marekebisho.
Upande wa wajibu pingamizi, Wakili wa Lema, Kimomogoro na
Wakili wa Serikali, Timoth Vitalis kwa niaba ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
walidai kuwa kasoro zote zilizotajwa hazina athari na zinaweza kurekebishika.
Hata hivyo, Mahakama ilitupilia mbali hoja mbili za rufaa
kuwa hazina msingi na ikakubaliana na hoja moja ya pingamizi kwamba kulikuwa na
tofauti au kuchanganywa kwa vifungu hivyo vya sheria.
Katika uamuzi wake wa
Novemba 8, 2012, Mahakama ilisema kuwa
kisheria, hati ya muhtasari wa hukumu ni lazima ikubaliane na hukumu lakini
katika shauri hilo muhtasari wa hukumu ulikuwa haukubaliani na hukumu.
“Hukumu inarejea Kifungu cha 114 (1)-(7), (Sheria ya
Uchaguzi), lakini hati ya decree inarejea Kifungu cha 113 (1)- (7),” ilisema
Mahakama hiyo na kuongeza:
“Decree lazima ikidhi masharti ya Amri ya XX, Kanuni ya 6 na
7, za Mwenendo wa Mashauri ya Madai, Sura ya 33. Katika shauri hili na kukiuka
amri ya XX Kanuni ya 6 na 7, dosari hiyo
inaifanya hati hii isiwe halali.
Hata hivyo, mahakama ilisema kuwa inakubaliana na mawakili
wa wajibu pingamizi hilo kuwa kosa hilo linawezekana limetokana
na kuteleza kwa kalamu au kutokana na kosa la uchapaji.
“Kwa sababu hii linaweza kurekebishwa chini ya Kanuni
ya 111ya Kanuni za Mahakama,” ilisema
Mahakama na kumpa Lema siku 14 kufanya marekebisho ya dosari hizo na kufungua
tena rufaa hiyo.
No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA