WENYE VIRUSI VYA UKIMWI WATAKIWA KUJIANDIKISHA ILI WASAIDIWE.
WAKAZI wa Mtaa wa Kipunguni Manispaa ya Ilala, ambao
wanaishi na Virusi vya Ukimwi (VVU) wametakiwa kwenda kujiandikisha katika
ofisi za serikali za mtaa huo kwa ajili ya kusaidiwa huduma mbalimbali.
Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa mkutano wa hadhara,
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kipunguni, Praxeda Mkandara, alisema kwa
kawaida huwa kuna fungu la Sh300,000 linalotolewa na manispaa kwa ajili ya
kusaidia waathirika wa Ukimwi.
Alisema fungu hilo hutolewa kila baada ya miezi sita na
kwamba ili mtu asaidiwe anatakiwa kwenda na uthibitisho wa vyeti ambavyo
vinaonyesha kuwa anaishi na Viruisi vya Ukimwi (VVU).
Hata hivyo baadhi ya wakazi wa mtaa huo walitilia shaka
suala hilo kwa madai kuwa kutokana na hali ngumu ya maisha watu wengine
wanaweza kugushi vyeti ili waonekane wameathirika kwa lengo la kupatiwa
misaada.
“Watu wengi wamepigika na maisha ukisema mtu aje na cheti
wengine wanaweza kutumia nafasi hiyo kugushi vyeti ili wapate misaada,”alisema
mmoja wa wakazi hao Mbaga Zacharia.
Mwenyekiti huyo alisema wanazo taratibu mbalimbali na kwamba
huwa hawatoi misaada hiyo hadi wajiridhishe ili misaada iwafikie walengwa
husika.
Pia aliwataka wakazi ambao hawajui kusoma na kuandika
wajitokeze kwenye madarasa ya elimu ya watu wazima ili waweze kupatiwa elimu
hiyo.
Katika hatua nyingine, diwani wa Kata ya Kipawa, Bonnah
Kaluwa, akizungumza kwenye mkutano huo, aliwataka watu wanaotaka zabuni za
kufanya usafi kwenye mitaa mbalimbali ya kata hiyo wajiunge kwenye vikundi kama
vya wajane na vijana.
Alisema lengo lao ni kuhakikisha fedha hizo zinarudi kwa
wananchi wenyewe ili waweze kujipatia kipato.Diwani huyo pia alisema hivi sasa
waameanza ukarabati wa makaravati baada ya kupata fedha za mfuko wa jimbo ambazo
ni Sh7.5 milioni.
No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA