UPELELEZI WA KESI YA LULU BADO GIZANI.
UPELELEZI wa kesi inayomkabili Msanii wa filamu nchini,
Elizabeth Michael maarufu kama Lulu, anayekabiliwa na kesi ya mauaji katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, bado haujakamilika.
Hayo yalielezwa jana na Wakili wa Serikali, Keneth Sekwao
wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa na kuangalia kama upelelezi
utakuwa umekamilika au la.
Sekwao alidai mahakamani hapo kuwa, upelelezi haujakamilika
na kuomba ipangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, Hakimu Mmbando
aliiahirisha kesi hiyo hadi Desemba 17, mwaka huu. Lulu anatuhumiwa kumuua
msanii mwenzake, Steven Kanumba. Anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 7, 2012
nyumbani kwa marehemu, Sinza Dar es Salaam.
Hata hivyo, umri wake ulizua mvutano mkali baina ya upande
wa mashtaka katika kesi hiyo na jopo la mawakili wanaomtetea, mvutano ambao
ulianzia Mahakama ya Kisutu na kuendelea hadi Mahakama ya Rufani, huku kesi ya
msingi ikiwa haijaanza kusikilizwa.
Juni 11, mwaka huu Mahakama Kuu ilikubali kufanya uchunguzi
wa umri halali wa mshtakiwa, kufuatia maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo
na jopo la mawakili wanaomtetea Lulu.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali,
Elizabeth Kaganda, akisaidiana na Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro
waliwasilisha maombi Mahakama ya Rufani wakiomba ifanye marejeo ya uamuzi wa
Mahakama Kuu, kama ulikuwa sahihi.
Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani lililoongozwa na
January Msoffe, Jaji Bernard Luanda na Edward Rutakangwa, lilizima mvutano na
likaamuru kuendelea kwa kesi ya msingi.
Katika uamuzi uliosomwa na Naibu Msajili wa Mahakama ya
Rufani, Zahra Maruma, jopo hilo kwanza lilisema maombi ya marejeo ya uamuzi wa
Mahakama Kuu, yaliyowasilishwa na Jamhuri yalikuwa batili.
No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA