BANGI MAGUNIA 97 YAKAMATWA NA JESHI LA POLISI JIJINI ARUSHA.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi
Liberatus Sabas akiwaonyesha waandishi wa habari madawa ya kulevya aina ya
bangi ambayo yalikuwa kwenye magunia 97 yaliyokamatwa na askari wa jeshi hilo
katika eneo la Usa river wilayani Arumeru.
Askari wa jeshi la polisi wakiwa wanashusha magunia ya
madawa ya kulevya aina ya bangi mara baada ya kukamatwa eneo la Usa River
wilayani Arumeru yakiwa yanasafirishwa kwenye gari aina ya Fuso lenye namba za
usajili T.282 AAJ kuelekea Moshi
Jeshi la Polisi mkoani hapa limemkamata mtu mmoja akiwa na
magunia 97 ya madawa ya kulevya aina ya bangi ambayo yalikuwa yanasafirishwa
toka mkoani hapa kuelekea Moshi. Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi Liberatus Sabas amesema
kwamba, tukio hilo lilitokea muda wa saa 10:00 alfajiri eneo la Usa River
wilayani Arumeru.
Alisema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati
ya jeshi hilo na wananchi ambapo taarifa za tukio hilo zilitolewa na raia wema
ambapo askari wa jeshi hilo waliweka mtego eneo hilo na kufanikiwa kulikamata
gari aina ya Fuso lenye namba za usajili T. 282 AAJ.
Kamanda Sabas aliongeza kwa kusema kwamba, ndani ya bodi ya
gari hilo kulikuwa na mboga aina ya kabeji iliyosambazwa vizuri huku chini ya
mboga hiyo kukiwa na madawa hayo yaliyokuwa kwenye magunia huku yakivingirishwa
kwenye mifuko ya “plastiki” kwa ndani.
Alisema katika gari hilo kulikuwa na watu watatu na mara
baada ya askari hao kulisimamisha dereva pamoja na msaidizi wake walifanikiwa
kukimbia huku mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Praygod Marick (22) Mkazi wa
Dar esalaam akikamatwa.
Jeshi la polisi Mkoani hapa linaendelea kumhoji mtuhumiwa
huyo huku watuhumiwa wengine wakiendelea kutafutwa. Kwa mara nyingine tena
Kamanda huyo aliendelea kuwashukuru wananchi wa Mkoa huu kutokana na
ushirikiano wao mkubwa wanaoutoa kwa jeshi hilo na kuendelea kuwasisitizia
kuimarisha mahusiano na jeshi hilo.
Kwa muda wa kipindi cha mwezi mmoja toka januari 07, 2013
mpaka hivi leo jeshi hilo limeshakamata madawa ya kulevya aina ya mirungi
magunia 372 katika magari mawili tofauti na pia limeshakamata jumla ya magunia
117 ya madawa ya kulevya aina ya bangi ambapo mwanzoni mwa wiki hii jumla ya
magunia 20 yalikamatwa yakiwa yanasafirishwa kwa kutumia wanyama aina ya Punda
maeneo ya Losoiti wilayani Longido.
Habari zaidi Libeneke la Kaskazini.

No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA