BAADA YA MAUWAJI MAKUBWA YA WANAFUNZI 20, RAIS OBAMA ATOA TAMKO.
Kufuatia moja kati ya mauaji makubwa kutokea katika
historia ya Marekani, wanasiasa akiwemo Rais Barack Obama, wametaka sheria
kuhusu umiliki wa bunduki nchini Marekani zibadilishwe, ili kuepusha maafa kama
hayo siku za usoni.
Akizungumza baada ya mauaji ya watoto na watu wazima 26
katika shule moja ya msingi katika jimbo la Connecticut Ijumaa, Rais Obama
aliyeonekana kujawa na huzuni, alitoa wito kuchukuliwe hatua ya maana kuzuwia
mauaji kwa kutumia bunduki.
Hakutoa maelezo zaidi.
Taarifa zaidi zimejitokeza kuhusu yaliyotokea katika mauaji
hayo katika shule ya msingi ya Sandy Hook mjini Newtown.
Mshukiwa mwenye umri wa miaka 20 - aliyeitwa Adam Lanza -
alimuuwa mama yake nyumbani kwake, kabla ya kuelekea katika shule hiyo na kuwafyatulia
risasi wanafunzi.
Walioshuhudia walisema walisikia zaidi ya milio mia moja ya
risasi na kuwaona watoto waliokuwa wakihofia maisha yao wakilikimbia jengo.
Wanafunzi hao walikuwa kati ya umri wa miaka mitano na kumi.
Wakaazi wa Newton wamekesha wakiomboleza.
Rais Obama ametoa amri kuwa bendera zipepee nusu mlingoti
kwenye majengo ya taifa.
Akizungumza juu ya mauaji hayo, waziri mkuu wa Australia,
Julia Gillard, alisema tukio hilo limezidi kusikitisha kwa vile waliouwawa ni
watoto.
Source: BBC Swahili

No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA