VIPODOZI HATARI VYATEKETEZWA TANI NZIMA NA TFDA.
MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA) katika Kanda ya Ziwa,
imekamata vipodozi vyenye viambato vinavyoathiri afya za watumiaji katika
Wilaya ya Bunda, mkoani Mara.
Vipodozi hivyo vina
thamani ya zaidi ya Sh10 milioni na tayari vimeteketezwa kwa moto.
Mkaguzi wa Dawa katika mamlaka hiyo Kanda ya Ziwa, Mtani
Njegere, alisema vipodozi hivyo vilikamatwa juzi katika maduka mbalimbali ya
mjini Bunda.
Njegere alisema vipodozi hivyo vilikuwa na uzito wa zaidi ya
tani moja na thamani yake ni zaidi ya Sh10 milioni.
Alisema vipodozi hivyo vimeteketezwa chini ya vyombo vya
ulinzi na usalama wilayani humo. Aliongeza kuwa TFDA katika kipindi cha wiki tatu mfululizo, imefanya zoezi hilo
mkoani humo.
“Kwa muda wa wiki tatu tumeendesha zoezi hili katika wilaya
zote za Mkoa wa Mara, tumefanikiwa kukamata vipodozi vilivyopigwa marufuku na
Serikali,” alisema.
Alisema katika wilaya nyingine hawakufanikiwa kuvikamata
vipodozi hivyo kutokana na wafanyabiashara kuvificha.
Alisema kuwa wafanyabiashara waliokamatwa na vipodozi hivyo
walionywa baada ya kujitetea kwamba walivinunua bila ya kujua.
Mkaguzi huyo alitoa wito kwa wananchi hususan wanawake, kuwa
makini wanaponunua vipodozi madukani,
kwa sababu vingi ni feki na tayari vimepigwa marufuku.
Alisema kutokana na hali hiyo, TFDA imeweka dira ya miaka
mitano kwa ajili ya kukabiliana na tatizo hilo.
Ofisa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Nashoni
Stafa, na Ofisa mifugo katika halmashauri hiyo, Rick Kaduri, walisema zoezi
hilo linapaswa kuwa endelevu kwa kuzingatia kuwa bidhaa feki zimezagaa kila
kona.

No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA