Mwalimu aua Mwanafunzi kwa kisu Handeni Mkoani Tanga.
![]() |
| Wanafunzi wakiwa darasani huku wamekaa chini . |
Mwalimu wa Shule ya Msingi Kwamwachalima, iliyopo katika
Kijiji cha Kwamwachalima Kata ya Komkonga wilayani Handeni Mkoa wa Tanga,
ametoweka baada ya kutuhumiwa kufanya mauaji ya kinyama kwa mwanafunzi wa
darasa la tatu na kumjeruhi vibaya mwingine wa kidato cha pili.
Mwalimu huyo, Suhalungi Nangoma (23) anatafutwa na Polisi
kwa tuhuma hizo
za kuua na kujeruhi kwa kisu wanafunzi hao ambao ni ndugu,
na watoto wa mwalimu mwenzake, Ijumaa Mjaliwa.
Nangoma anatuhumiwa kumuua kwa kumchoma kisu kifuani binti
huyo anayesoma darasa la tatu katika shule hiyo, Farihia Mjaliwa (9), kisha
kumjeruhi kwa kumcharanga kisu tumboni
kaka wa binti huyo, Mohamed Farhia anayesoma kidato cha pili katika
Sekondari Kisaza.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Jafari Mohamed
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema polisi wanaendelea kumsaka
mtuhumiwa ili afikishwe mahakamani.
Taarifa zilizopatikana kutoka katika eneo la tukio na
kuthibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu zilieleza kuwa
tukio hilo lilitokea saa 9:00 usiku Novemba 23, mwaka huu wakati mtuhumiwa
alipowavamia watoto hao chumbani kwao na kuanza kuwashambulia kwa kisu. Baba mzazi
wa watoto hao, Mjaliwa anafundisha shule moja ya Kwamwachalima anasema
hawakuwahi kugombana.
Mtuhumiwa huyo ametenda kosa hilo huku akikabiliwa kesi ya
kumpachika mimba mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya
Kisaza.
Akisimulia mkasa uliowakuta watoto wake mbele ya mkuu wa
wilaya, Mjaliwa alisema Mohamed ambaye alinusurika kifo, alichomwa kisu tumboni
na kusababisha utumbo kutoka nje na kwamba sasa amelazwa katika Hospitali ya
Wilaya ya Korogwe, Magunga.
Kwa mujibu wa Mjaliwa, mtuhumiwa baada ya kufanya kitendo
hicho alimgeukia mdogo mtu na kisha kumchoma kisu kifuani upande wa kushoto na
kukiacha kikining’inia.
“Watoto hao walianza kupiga kelele kutoka na mashambulizi
hayo, lakini mtuhumiwa alitimua mbio na kukimbilia kusikojulikana,” alisema
Mjaliwa ambaye hakuwepo siku ya tukio.
“Cha kushangaza alikuwa nje kwa dhamana kwa kumpa mimba
mwanafunzi,” alisema.
Habari zinadai kuwa siku ya tukio, baadhi ya walimu wa Shule
ya Kwamwachalima walifanya kikao kifupi kujadili jinsi ya kumwekea dhamana
Nangoma, iwapo angefikishwa mahakamani kwa kesi ya kumpachika mwanafunzi mimba.
Mwenyekiti wa Kamati ya Shule hiyo Ali Hatibu, alisema
walimhoji majeruhi huyo kabla hajapoteza fahamu na kumtaja mwalimu huyo kwamba
ndiye aliyemchoma kisu.
“Tuliingia chumbani kwa watoto na kukuta kumetapakaa damu
nyingi, lakini binti huyu ambaye sasa ni marehemu tulikuta tayari ameshafariki
dunia na alikuwa ameshikilia kisu, maana alichomwa kwenye moyo,” alisema
Hatibu.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Kwamwachalima, Eva Msenga alisema
kwamba siku ya tukio mchana alizungumza na mtuhumiwa baada ya kuona mwenendo
wake hauridhishi na kwamba alimjibu kwamba alikuwa amechanganyikiwa kutokana na
kesi inayomkabili.
Msenga alisema baadaye jioni alikuwa na watoto hao
wakijisomea hadi saa tatu usiku, na kwamba muda huo aliwataka wakalale kwani
muda ulikuwa umekwenda.
“Tuliagana na waliondoka kwenda kulala, baadaye usiku ndipo
tuliposikia tukio hili na tuliambiwa kwamba mtuhumiwa alibisha hodi na watoto kwa
kumfahamu walimfungulia kisha akawafanyia unyama huo wa kutisha,” alisimulia
Msenga.
Rweyemamu akizungumza wakati akiwafariji wanafamilia hao
alisema Serikali itachukua hatua za kumsaka mtuhumiwa popote alipo ili aweze
kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Alisema hatua ya kwanza ambayo ofisi yake imechukua ni
kuomba kufungwa kwa akaunti za mtuhumiwa na kwamba hilo linaweza kuwa msaada wa
kunaswa kwake.
“Tutafanya kila namna kuhakikisha kwamba mwalimu huyu
anakamatwa ili apambane na mkono wa sheria,” alisema mkuu huyo wa wilaya.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Jafari Mohamed
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba polisi wanaendelea kumsaka
mtuhumiwa ili afikishwe mahakamani kwa kosa la mauaji.
Source: Mwananchi

No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA