TAIFA STARS YAICHAPA HARAMBEE STARS CCM KIRUMBA JIJINI MWANZA.
Beki wa timu ya Taifa ya Tanzania
'Taifa Stars', Aggery Morris (kulia) akifunga bao la kichwa wakati wa mechi ya
kirafiki ya Kimataifa dhidi ya Harambee Stars ya Kenya kwenye Uwanja wa CCM Kirumba
Mwanza jana. Picha na Fidelis Felix.
BAO la Aggrey Morris lilitosha kuipa Taifa Stars ushindi wa
bao 1-0 dhidi ya Harambee Stars ya Kenya katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa
uliofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Morris alifunga bao hilo
pekee katika dakika 7 akiunganisha kwa kichwa kona iliyopigwa na Amir Maftah.
Kwa matokeo hayo Stars imefanikiwa kulipa kiasi cha kufungwa
mabao 2-1 kwenye uwanja huo na Kenya mwaka 2009.
Akizungumza baada ya mechi kumalizika kocha wa Taifa Stars,
Kim Poulsen alisema amefurahishwa na ushindi alioupata.
"Taifa Stars ilikuwa haijakaa pamoja kwa muda wa miezi
mitatu iliyopita, hivi sasa ndiyo tumepata nafasi ya kujiandaa kwa muda wa siku
mbili na kucheza mechi hii, naamini wachezaji wanastahili pongezi kwa ushindi
tulioupata,"alisema Poulsen.
Alisema,"tutatumia muda tulionao kujiandaa, kwani
tumeweka kambi hapa Mwanza kwa ajili ya kujiandaa, naamini muda tulionao hivi
sasa unatosha kuiandaa timu, siku zote maandalizi ndiyo kitu muhimu."
Naye kocha wa timu ya taifa ya Kenya 'Harambee Stars', Henry
Michel alisema,"sijafurahishwa na mechi hii, kiwango
hakijaniridhisha."
Taifa Stars ilianza mchezo kwa kasi na dakika ya kwanza
Ngassa alipiga shuti la mbali lililotoka nje kidogo ya goli, nao Kenya walijibu
mapigo kupitia Denis Oliech aliyekosa bao la wazi akiwa yeye na kipa Juma
Kaseja.
Stars ilipata bao la kuongoza katika dakika 7 kupitia
nahodha wake msaidizi Morris aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa
na Maftah.
Baada ya bao hilo Taifa Stars iliendelea kupeleka
mashambulizi katika lengo la Harambee Stars, ambapo mshambuliaji wa Thomas Ulimwengu wa Taifa Stars alipoteza
nafasi mbili za wazi za kufunga katika dakika 13 na 14 akiwa yeye na kipa kwani
mashuti yake yalitoka nje.
Vilvile Mrisho Ngasa na Mbwana Samata waligongea pasi na kuwatoka
walinzi wa Kenya, lakini kipa wa Kenya, Fredrick Onyango alikuwa makini kuokoa
hatari hiyo.
Katika mchezo huo Kelvin Yondani, Samata na Morris
walionyeshwa kadi za njano kutokana na makosa mbalimbali waliyoyafanya.
Stars ilicheza vizuri katikati ya uwanja, ambapo viungo
Abubakari Salum, Frank Domayo na Mwinyi Kazimoto walifanya kazi kubwa ya
kutuliza mpira na kugongeana pasi fupi fupi za chini na kupitisha mipira mizuri
kwa Ulimwengu, Samata na Ngassa waliokuwa mwiba kwa ngome ya Harambee Stars
kutokana na kasi yao.
Kenya wenyewe walitumia zaidi mipira ya juu kuwapitishia
Oliech, Ugine Sike na Edwin Wafula waliotumia vizuri urefu wao kucheza mipira
ya juu.
Kocha wa Kenya, Michel aliwapumzisha Jerry Santo, Patrick Obaya
na Jonas Stima na kuwaingiza Christopher Wekesa, Timbe Ayoub na Antony Akumu.
Naye Kim aliwatoa Kazimoto, Ngasa, Samata, Ulimwengu, Maftah
na kuwaingiza Amri Kiemba, Simon Msuva, Christopher Edward, John Bocco na
Shaban Nditi.
Mabadiliko hayo hayakuweza kubadilisha mchezo huo kwani
washambuliji wa Stars walipoteza nafasi kadhaa za kufunga wakiwa wao na kipa
Onyango aliyekuwa kikwazo kikubwa kwao.
Taifa Stars itaendelea na kambi yake jijini Mwanza kujiandaa
na mashindano ya Chalenji yatakayoanza Novemba 24, jijini Kampala.
Vikosi
Taifa Stars
Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Amir Maftah, Kelvin Yondani,
Aggrey Morris, Frank Domayo, Abubakari Salum, Mwinyi Kazimoto, Thomas
Ulimwengu, Mbwana Samata na Mrisho Ngassa.
Harambee Stars
Fredrick Onyango, Brian Mandela, Ugine Asike, Jonas Stima,
Edwin Wafula, Jerry Santo, Jerry Opiyo, Patrick Oboya, Patrick Osiako, Denis
Oliech na Wisley Keman.
Source:Mwananchi

No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA