Tume ya Mabadiliko ya Katiba: Ukusanyaji wa Maoni Awamu ya Nne Unaendelea.
Jumatano, Novemba 14, 2012
Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatarajia kuendelea na awamu
ya nne na ya mwisho ya mikutano yake na wananchi wa mikoa sita kuanzia siku ya
Jumatatu, Novemba 19, 2012 hadi Jumatatu, Desema 19, 2012 kwa lengo la
kukusanya maoni yao kuhusu Katiba Mpya.
Mikoa hiyo ni Dar
es Salaam, Arusha, Simiyu, Geita, Mara na Mjini
Magharibi na kila siku kutafanyika mikutano miwili, wa kwanza utaanza saa 3:00
asubuhi – saa 6:00 mchana na kufuatia na mwingine utakaoanza saa 8:00 alasiri –
saa 11:00 jioni.
Taratibu zote za kuanza kazi ya kukusanya maoni katika mikoa
iliyotajwa zimekamilika zikiwemo kuandaa ratiba na kuisambaza katika ofisi za
mikoa, wilaya na Halmashauri za Manispaa na Wilaya husika. Wajumbe wa Tume na
watumishi wa Sekretarieti wamejigawa katika makundi saba. Kila mkoa utakuwa na
kundi moja isipokuwa Dar es Salaam
ambao utakuwa na makundi mawili.
Katika mkoa wa Dar
es Salaam Tume imejigawa katika makundi mawili na siku
hiyo ya Jumatatu itaanza na Wilaya za Temeke na Ilala. Katika wilaya ya Temeke,
Tume itaanza na eneo la Keko wakati katika wilaya ya Ilala itaanza na eneo la
Jangwani kwa mikutano itakayoanza saa 3:00 asubuhi. Kwa mikutano ya alasiri,
wilayani Temeke mkutano huo utafanyika Chang’ombe na ule wa Ilala utafanyika
Tabata.
Kwa upande wa mkoa wa Arusha, Tume itaanza na Wilaya ya
Karatu eneo la Mbulumbulu wakati mkoani Mara Tume itaanza katika Wilaya ya
Tarime eneo la Bumera. Kwa mkoa wa Simiyu, Tume itaanza na Wilaya ya Busega
eneo la Lamadi na mkoani Geita, Tume itaanza na Wilaya ya Chato eneo la Kachwamba.
Kwa mkoa wa Mjini Magharibi, Tume itaanza katika Wilaya ya Magharibi.
Tume inawaomba wananchi kuhudhuria mikutano itakayoitishwa
na Tume na kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni yao kwa kuzungumza na pale
wanapokosa nafasi ya kuzungumza, watumie fursa ya kuwasilisha maoni yao kwa
maandishi kwa kutumia fomu maalum zitakazokuwa zinatolewa na Tume katika
mikutano hiyo.
Pamoja na kuwasilisha maoni kupitia mikutano itakayoitishwa
na Tume, wananchi pia wanaweza kuwasilisha maoni yao kupitia tovuti ya Tume (www.katiba.go.tz)
au kwa njia ya posta kupitia anuani za zifuatazo:
Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Makao Makuu,
Mtaa wa Ohio,
S.L.P. 1681,
DAR ES SALAAM,
Simu: +255 22
2133425,
Nukushi: +255 22
2133442;
Au
Jengo la Ofisi ya Mfuko wa Barabara, Mtaa wa Kikwajuni Gofu,
S.L.P. 2775, Zanzibar, Simu: +255 224 2230768, Nukushi: +255 224 2230769
Tume inawaomba wananchi kuhudhuria mikutano itakayoitishwa
na Tume na kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni yao kwa uwazi, uhuru na
utulivu.
Mwisho.
Imetolewa na:
Assaa Rashid,
Katibu,
Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
S.L.P. 1681,
DAR ES SALAAM
+255 (0) 0757 500 800 / 0717 084 252

No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA