CCM WAMHUSISHA KARUME NA KIKUNDI CHA UAMSHO.
![]() |
|
RAIS Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Aman
Karume
|
RAIS Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Aman
Karume juzi usiku alizomewa na baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), huku wakimwita kwamba ni mmoja wa wanakundi la Uamsho.
Uamsho ni kundi ambalo katika siku za hivi karibuni limekuwa
likihusishwa na vurugu ambazo zimekuwa zikitokea Tanzania Visiwani, ambazo
zimesababisha watu kadhaa kukamatwa na kufikishwa mahakamani.
Rais Karume alikutana na zahama hiyo wakati akitoa hotuba ya
kuwaaga wanaCCM baada ya kumaliza ngwe yake ya utumishi ndani ya chama hicho
akiwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar.
Dalili za Rais Karume kuzomewa zilianza baada ya baadhi ya
wajumbe kutoka Mkoa wa Mjini Magharibi kuanza kutaja neno ‘Uamsho’ kila
alipokuwa akizungumzia matatizo yaliyopo Zanzibar.
Hali ilikuwa mbaya zaidi pale alipokuwa akizungumzia vurugu
za kidini ambazo ziliikumba Zanzibar hivi karibuni zikiongozwa na kikundi cha
Uamsho.
Karume alisema kuwa kikundi cha Uamsho kina haki ya kutoa
maoni yake kuhusu muungano, lakini hakipaswi kufanya vurugu kama ambavyo
kimekuwa kikifanya.
Wakati akiendelea kuzungumzia suala hilo, kelele nyingi
zilienea katoka kwa wajumbe wa mikoa ya Zanzibar ambao walikuwa wakipaza sauti,
“ Uamsho huyo….Uamsho huyo… Uamsho huyo….”
Hali hiyo ilimfanya wakati mwingine kukatiza hotuba yake na
kulazimisha kuwatuliza watu hao kwa kusema “CCM
oyeee….CCM…..oyeee…Mapinduziii….”
Hata hivyo, baada ya kelele hizo kuendelea Karume alionekana
kuhamaki na kuwaambia wajumbe hao kwamba amechoka kusikia akiitwa jina hilo la
Uamsho.
“Nimechoka kusikia naitwa jina hilo ati,” alisema Karume na
kuongeza:
“Hivi wengine wana vichwa vya samaki kwa nini mnapiga kelele
wakati mimi ninapozungumza, si mniache nizungumze mambo ambayo ni muhimu zaidi
kwa masilahi ya chama chetu.”
Hata hivyo, licha ya kutafuta namna ya kuwatuliza wanachama
hao kwa maneno mengi na historia ya maisha yake tangu alipojiunga na Chama cha
ASP mwaka 1970, bado hakukuwa na utulivu na safari hii kelele zilianza kwa
pande zote za wajumbe.
Kwa upande wa wajumbe wa Bara, baadhi yao walikuwa wakipiga
kelele za kumtaka kumaliza hotuba yake ambayo walisema ilishachukua muda mrefu
huku wakisema hakuna cha ajabu alichokuwa akizungumza.
Mara baada ya kumaliza hotuba yake, Karume alihojiwa na
Idhaa ya Kiswahili ya Redio Deutche Welle ya Ujerumani, na alisisitiza kuwa
Uamsho wana haki ya kutoa maoni yao kuhusu muungano, lakini hawaruhusiwi
kuvunja sheria.
Aliwataka wanachama wa kikundi hicho kujenga hoja, kwani
alisema wengine wana hoja za msingi, lakini wasitumie vitisho.
Karume alistaafu uongozi wa CCM katika nafasi ya Makamu
Mwenyekiti (Tanzania Visiwani) na nafasi yake ilichukuliwa na Rais wa sasa wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein.
Tofauti na utamaduni ambao CCM kimeujenga kwa viongozi wake
wakuu, Karume aliendelea kuwa makamu mwenyekiti hata baada ya kustaafu urais wa
Zanzibar, hivyo kumlazimisha Dk Shein kusubiri hadi juzi kuchukua nafasi hiyo.
Kwa kawaida, viongozi wa ngazi ya Rais wa Muungano na
Zanzibar, baada ya kuondoka katika nafasi zao za uongozi wa nchi, pia huachia
madaraka ndani ya chama na kumwachia Rais mpya.
Source:Mwananchi

No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA