LOWASA AENDA UJERUMANI KWA MATIBABU
Asili Yetu Tanzania.Copyright
![]() |
| Edward Lowasa |
ALIYEKUWA Waziri Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Nne,
Edward Lowassa yupo nchini Ujerumani kwa matibabu na uchunguzi wa kiafya.
Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli jana hakuwapo katika
uzinduzi wa mradi wa Barabara ya Minjingu hadi Arusha na shule jimboni kwake,
uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete aliye ziarani mkoani Arusha.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa
Wilaya ya Monduli, Jowika Kasunga na baadaye kusambazwa kwa waandishi wa
habari, Lowassa alieleza kusikitishwa kutokuwapo jimboni kwake wakati huo ambao
Rais Kikwete anatembelea jimbo lake.
Lowassa alisema kuwa, hali hiyo imetokana na kuwa safarini
kwa ajili matibabu lakini akasema anaamini mambo yataenda vizuri si kwa ziara
hiyo ya Rais Kikwete bali hata vikao vya juu vya CCM vinavyotarajiwa kufanyika
hivi karibuni.
Katika taarifa hiyo, alimsifu Rais Kikwete kuwa, kutokana na kutekeleza
vizuri na kwa uadilifu Ilani za uchaguzi za CCM, wiki mbili zijazo wanaCCM
watakwenda Dodoma
kuidhihirishia dunia na Watanzania wenye
shaka kwamba wanamwamini na kuuthamini uongozi wake.
Katika maelezo hayo, Lowassa alieleza tatizo linalomsumbua
kuwa ni macho, lakini pia atatumia nafasi hiyo kuchunguza afya yake.
Aidha, alimshukuru Rais Kikwete kwa kuzindua miradi hiyo
akisema inadhihirisha mambo mawili makubwa aliyoyafanya kwa kiwango cha juu
chini ya uongozi wake akiwa Rais wa Tanzania.
“Mosi, chini ya uongozi wako shule nyingi zaidi zimejengwa
kuliko awamu zote zilizotangulia. Pili, kilomita za barabara za lami
zilizoongezeka wakati wa awamu yako ni ndefu kuliko wakati mwingine wowote,”
alisema Lowassa na kuongeza:
“Kwa hakika umetekeleza vizuri, kikamilifu na kwa uadilifu
Ilani za uchaguzi za CCM, mwaka 2005 na 2010. Sisi wanachama wa CCM na wananchi
wa Monduli ni mashahidi wa jambo hili. Tunaamini ndivyo ilivyo kwa nchi nzima.”
Mwishoni mwa wiki ijayo CCM itafanya uchaguzi mkuu wa
uchaguzi ngazi ya taifa kuanzia mwenyekiti wa chama na viongozi wengine, ili
kukamilisha kupanga safu mpya ya uongozi kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2015.
CCM ipo katika uchaguzi wa ndani wa chama hicho ambapo
tayari jumuiya zake za Wazazi, Vijana na Wanawake zimekamilisha chaguzi hizo,
huku kambi ya Lowassa ikitajwa kuibuka kidedea kwa kunyakua nafasi mbalimbali
zilizowaniwa, kuanzia ngazi za wilaya hadi jumuiya za chama kitaifa.
Katika uchaguzi wa UWT, Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Taifa,
Sophia Simba ambaye alitetea nafasi yake na Makamu wake, Asha Bakari Makame
wanatajwa kuwa wafuasi wa Lowassa, huku wajumbe sita kati ya wanane waliochaguliwa kuwakilisha jumuiya hiyo
katika Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho, wakiwa waumini wa kambi
hiyo.
Wajumbe sita kati ya wanane walioshinda nafasi za ujumbe wa
NEC kupitia jumuiya hiyo wanatajwa kuwa
wafuasi wa Lowassa, huku mmoja akitajwa
kuwa hana kundi lolote huku mwingine akitajwa kumuunga mkono aliyekuwa mgombea
wa uenyekiti wa UWT na Mbunge wa Same Mashariki, Anne Killango Malecela.
Kwa upande wa UVCCM, Mbunge wa Donge, Sadifa Juma Khamisi
ambaye alichaguliwa kuwa Mwenyekiti kwa kura 483 na makamu wake, Mboni Muhita
pia wanatajwa kuwa wafuasi wa kambi ya Lowassa.
Waliotwaa ujumbe wa NEC na ujumbe wa Baraza Kuu la Umoja
huo, pia wanatajwa kuwa waumini wa kambi hiyo.
Hata hivyo, katika uchaguzi wa Jumuiya ya Wazazi uliokuwa wa
funga dimba la mfululizo wa chaguzi za chama hicho tawala kuanzia ngazi za
shina tangu Aprili, waliokuwa wagombea wa nafasi ya uenyekiti, John Barongo na
Abdallah Bulembo kwa nyakati tofauti walikanusha kuwa na masilahi na makundi
huku Martha Mlata akikataa kuzungumzia uchaguzi huo.
Rais Kikwete
Akizungumza katika hafla hiyo, Kikwete alisema kwamba ni
lazima barabara zote ziwekwe matuta ili kuzuia ajali za barabarani, akieleza
kuwa mara nyingi baada ya ujenzi wa barabara, kinachofuatia ni vifo
vinavyotokana na tabia ya madereva wakorofi.
MWANANCHI

No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA