Header Ads

Breaking News
recent

KIKWETE: WANAOUTAKA URAIS WANAKIVURUGA CHAMA.

Mwenyekiti wa CCM - Rais Jakaya Kikwete.

MWENYEKITI wa CCM, Rais Jakaya Kikwete amesema mpasuko uliopo ndani ya chama hicho unatokana na makundi yanayotaka uongozi wa juu ikiwamo nafasi za urais mwaka 2015.
Aidha, amesema hana kundi lolote analoliunga mkono ndani ya chama hicho na kuwataka wanaotaka aingie katika makundi yao wamwache.

Akifungua Mkutano Mkuu wa Nane wa CCM katika Ukumbi wa Kizota nje kidogo ya Mji wa Dodoma, Rais Kikwete alisema ukiondoa mpasuko unatokana na kuwania madaraka, hali ndani ya chama hicho ni shwari.

“...Chama bado kiko imara, ukiacha makundi hayo ambayo hata mimi wananilazimisha niwe kwa baadhi ya kundi na mimi nikawaambia siwezi kuwa katika kundi moja maana mimi ni mwenyekiti, itakuwaje katika kikao cha uamuzi?” alisema.

Katika hotuba yake iliyochukua saa 1:48, mwenyekiti huyo alisema, anazo taarifa na hata kujionea kwa macho kuwa uamuzi wa baadhi ya wanaCCM kugombea madaraka, ndiyo unaosababisha migogoro ndani ya chama.

“Nikiwauliza kama nani anajua migogoro ndani ya chama chetu kuwa ipo mtajibu nini? Nawahakikishia kuwa inatokana na watu wanaoutaka uongozi ikiwamo kutangaza nia za urais, ubunge na udiwani.”

Alisema robo tatu ya migogoro yote ya ndani ya CCM inatokana na watu kutaka vyeo, lakini akasema kufanya hivyo si dhambi na wala wanaowaunga mkono watu wengine wasihesabiwe kuwa watenda dhambi.

Mwenyekiti huyo alisema watu wanapotangaza ni zao, kumekuwa na malumbano na migongano inayosababisha kutokuelewana jambo alilokemea akisema halifai kuwapo, kwani linaelekea kukimomonyoa chama hicho.

Hata hivyo, aliwataka wanaotangaza nia, kuishia kuonyesha dhamira zao na wasithubutu wala kujaribu kukiua chama akiwatishia kuwa nao hawatabaki salama.
Alisema wenye ndimi mbili hawapaswi kuwapo ndani ya chama akisema watatimuliwa wakatafute maeneo mengine katika vyama vingine ambako wanaamini watapata nafasi.
Aliwataka wapambe wa wagombea kuacha kuendeleza migogoro akijitolea mfano kwamba alikuwa na wapambe wakati anawania urais, lakini wote walibaki kitu kimoja.

Takukuru wajazana
Maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), jana walijazana katika mkutano huo wakiwasaka watu wanaotoa rushwa kwa wajumbe.
Maofisa hao wakiwa wamevalia sare za CCM walionekana katika maeneo yote muhimu ambayo yangeweza kutumika kutolea rushwa ikiwamo vyooni , sehemu ya chakula na vinywaji.

Wapambe wa Membe wafunika
Kikosi cha wapambe wa mgombea wa nafasi ya Nec Bara, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano na Kimataifa, Bernard Membe jana walitawala katika Ukumbi wa Kizota wakiimba nyimbo mbalimbali za kumsifia mgombea huyo.

“Chagua Membe…Chagua Membe…Hakuna kama Membe… hakuna kama Membe…. Chagua Membe, Chagua Membe… ,” waliimba huku wakiwa na karatasi kubwa walizovaa kifuani zilizobeba wasifu wa Membe na picha yake.

Wapambe hao ambao waliingia katika viwanja vya ukumbi huo saa 2:00 asubuhi walifanya wajumbe waliokuwa wamefika katika eneo hilo kuwaangalia.

Mitindo ya wapambe wagombea jana ilibadilika baadhi yao wakipiga magoti katika maeneo wanayopita wajumbe wa mkutano mkuu wakati wa mapumziko na kunyoosha mikono juu kuomba wawapigie wagombea wao.
Huku wakiwa wamening’iniza karatasi zenye picha na wasifu wa wagombea wao kifuani.

Mmoja wa wapambe wa wagombea hao alionekana kupiga magoti akiwasihi wajumbe kumpigia kura mgombea wa Nec, January Makamba.

Katika hatua nyingine, baadhi ya wajumbe wa mkutano huo juzi walikosa mahali pa kulala kutokana na nyumba za wageni walikopangiwa kujaa.

No comments:

KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA

Powered by Blogger.