MBOWE AMTAKA SUMAYE KUVUA GAMBA NA KUVAA GWANDA LA CHADEMA.
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na
kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe, amemtaka Waziri Mkuu
mstaafu, Fredrick Sumaye, kuacha kuendelea kulalamikia vitendo vya rushwa ndani
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na badala yake achukue hatua ya kuvua gamba na
kuvaa gwanda.
Mbowe ametoa ushauri huo kwa Sumaye jana wakati akihutubia
maelfu ya wakazi wa Katesh wilayani Hanang’ mkoani Manyara katika mkutano wa
hadhara kuhamasisha wananchi kupambania haki zao mara baada ya kutoka bungeni
mjini Dodoma.
”Nimeshangazwa sana hivi sasa suala la rushwa katika nchi
hii kuwa ni kilio cha kila mmoja, hata viongozi wakubwa katika nchi badala ya
kuchukua hatua nao wanalia kukithiri kwa vitendo vya rushwa vilivyoota mizizi
katika nchi hii, hususani ndani ya chama cha CCM.
“Namshauri Sumaye ambae amekuwa waziri mkuu wa nchi hii kwa
miaka 10 na mwaka huu kakumbana na dhoruba kubwa ya kubwagwa katika uchaguzi wa
CCM kwa kuzidiwa na nguvu ya rushwa na kubaki kulalamika bila kujua nini
anahitajika kufanya.
“Narejea tena kusema kama Sumaye anataka kuidhihirishia nchi
hii uadilifu wake, basi ni wakati sasa wa kuionyesha dunia kuwa anakerwa na
rushwa kwa kuamua kujiondoa ndani ya CCM na kujiunga na wanamapinduzi wenye
lengo la kuikomboa nchi hii kutoka katika lindi la wala rushwa.
”Mwanaume ukiishaangukia pua katika jambo lolote lile,
unatakiwa kuamka na kufuta vumbi na kisha kuamua kutoa maamuzi ya nini cha
kufanya na kusonga mbele, na sio kulalamika hivyo Sumaye amua moja; Vua Gamba
Vaa Gwanda,” alisema Mbowe.
Aidha, katika mkutano huo aliwataka wananchi kufikiria
maisha magumu wanayokabiliana nayo hivi sasa, yanayotokana na viongozi waliopo
madarakani kuamua kujilimbikizia mali wao na familia zao na kusahau vijana
wanaotoka familia masikini.
Alifafanua kuwa kutokana na matabaka kutawala katika nchi
hii, ya walionacho na wasionacho hali hiyo imeingia sasa katika sekta ya elimu,
ambapo sasa kuna matabaka ya shule za walionacho na wasionacho.
Alisema hali hiyo hivi sasa inaenda kuzalisha watoto wa
matajiri na viongozi kuandaliwa kuja kuendelea kuwatawala watoto wanaotoka
katika familia za walalahoi, ambao hawawezi kupata elimu bora kutoka katika
shule za binafsi zenye kutoa taaluma bora.
Katika mkutano huo, Mbowe alipokea wanachama waliojiengua
kutoka CCM na kuamua kujiunga na CHADEMA ambapo aliwataka walioamua kuvua gamba
na kuvaa gwanda wawe makamanda wa ukweli ndani ya chama hicho.
Na Ramadhani Siwayombe, Hanang’

No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA