IKULU: HATUWEZI KUMZUIA MHESHIMIWA MBUNGE TUNDU LISSU KUMSHTAKI RAIS.
Rais Jakaya Kikwete.
SIKU moja baada ya Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni,
Tundu Lissu kusema atawasilisha hoja ya kumshtaki Rais Jakaya Kikwete iwapo
atashindwa kuwaondoa kazini majaji wasio na sifa aliowateua, Ikulu imemwambia
aendelee na mchakato wake.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alisema
jana kuwa hakuna anayemzuia Lissu kushtaki kama
anaona kuna sababu za kufanya hivyo.“Lissu ni Mbunge na ana haki zake za msingi
na kama amefikia hatua hiyo anaweza kufanya
hivyo... hakuna mtu ambaye anaweza kumkataza. Nani mwenye uwezo wa kuingilia
uhuru wa mtu?”
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Bunge
jana, Lissu alisema amechukua uamuzi huo baada ya kuona Bunge limeikalia ripoti
ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge iliyomhoji kuhusu kauli yake ya
kuwatuhumu majaji kuwa baadhi yao
hawana sifa.
Alisema ameamua kuchukua hatua hiyo baada ya kuona Rais
Kikwete ambaye ana mamlaka ya kuteua majaji, ameshindwa kuwaondoa kazini majaji
hao wasiokuwa na sifa.
Lissu alisema atawasilisha hoja yake hiyo kwa kutumia Kanuni
ya Bunge sehemu ya 11, Ibara ya 121, 122, 123, 124, 125 na 126 na pia kwa
kutumia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 146 A.
Sehemu ya 11 ya Kanuni ya Bunge, Ibara ya 121 inaeleza kuwa
mbunge yeyote anaweza kuwasilisha kwa Spika taarifa ya hoja ya kumshtaki Rais
kwa madhumuni ya kumuondoa Rais madarakani kupitia azimio la Bunge kwa mujibu
wa Ibara ya 46 A ya Katiba ikiwa
inadaiwa kwamba Rais; ametenda vitendo ambavyo kwa ujumla vinavunja katiba au
sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
Lissu alisema atakusanya saini za wabunge kuunga mkono hoja
yake ambayo ni asilimia 20 kwa mujibu wa Kanuni za Bunge. Wabunge wote kikatiba
ni 357.
Julai 13, mwaka huu wakati akitoa maoni ya kambi ya upinzani
katika Wizara ya Katiba na Sheria bungeni, Lissu alisema uteuzi wa majaji
umegubikwa na ukiukwaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Alisema baadhi ya majaji walioteuliwa hawana sifa, uwezo na
kwamba hawakufaa kufanya kazi hiyo.
Kauli hiyo ilisababisha Bunge kuiagiza Kamati ya Haki,
Maadili na Madaraka ya Bunge inayoongozwa na Mbunge wa Mlalo (CCM), Hassan
Ngwilizi kumhoji ili athibitishe kauli yake.
Alisema wakati akihojiwa na kamati hiyo, pamoja na nyaraka
nyingine, aliwasilisha nakala ya ripoti ya kikosi kazi kilichoundwa mwaka 2008
na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika na aliyekuwa Katibu
Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo kuchunguza uteuzi wa majaji nchini.
Alisema ripoti ya kikosi kazi hicho kilibaini kuwapo majaji
ambao hawana sifa ya kufanya kazi hiyo, lakini Rais Kikwete ameshindwa
kuwaondoa kazini.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi
ya Chadema, alisema hali ya Mahakama ni mbaya, kwani kuna majaji wawili ambao
waliwahi kukamatwa kwa rushwa wakiwa mawakili, lakini wakateuliwa kufanya kazi
hiyo.
Alisema baadhi ya majaji hawana uwezo hata wa kuandika
hukumu kutokana na kutojua vyema lugha ya Kiingereza ambayo ndiyo inayotumika
katika Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani.
Alisema ili mtu aweze kuchaguliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu
lazima awe na elimu ya shahada ya kwanza ya sheria, awe ametumikia miaka 10
mahakamani na anayechaguliwa kuwa jaji wa Mahakama ya Rufani lazima awe
ametumikia miaka 15 mahakamani.
Mbali ya kueleza hayo, Lissu alisema kwamba alitoa pia
katika kamati hiyo, ushahidi unaoonyesha kuwa kuna jaji mmoja wa Mahakama Kuu
ambaye hawezi hata kuandika sentensi moja ya Kiingereza ilinyooka... “Kama jaji hawezi kuandika hata sentensi moja ya
Kiingereza ilinyooka, tunaweza vipi kuwa na Mahakama inayotenda haki?”
Alisema kuna jaji mwingine ambaye ameongezewa mkataba wa
kufanya kazi mara ya tatu kitu ambacho ni kinyume cha sheria. Alisema kwa
mujibu wa Tume ya Mahakama, hakuna jaji ambaye anaweza kufanya kazi kwa mkataba
kwa vipindi vitatu.
Kama Lissu atachukua hatua hiyo, itakuwa ni mara ya pili kwa
mbunge kuwasilisha bungeni hoja ya kutaka kumwajibisha kiongozi wa juu
serikalini.
Mara ya kwanza alikuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema),
Zitto Kabwe katika Bunge lililopita alipokusanya saini za wabunge kutaka kupiga
kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akitaka awawajibishe
baadhi ya mawaziri waliokuwa wametajwa kuhusika katika matumizi mabaya ya
madaraka katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Hata hivyo, Rais Kikwete alifanya mabadiliko makubwa katika
Baraza lake la Mawaziri hivyo kuzima hoja hiyo ya Zitto.
Gedius Rwiza


No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA