AJALI MBEYA YAUWA WATU SITA HAPO HAPO.
| BASI AINA YA TOYOTA HIACY YENYE NAMBA ZA USAJIRI T245 AMH ILIYOGANWGA NA ROLI LA MIZIGO |
JINAMIZI la ajali mkoani Mbeya limeendelea kumaliza roho za
watu baada ya watu sita kupoteza
maisha na wengine 10 kujeruhiwa katika
ajali iliyotokea eneo la Itewe, Kata ya Inyala, Wilaya ya Mbeya Vijijini.
| HILI NDILO ROLI LILILOSABABISHA AJALI NA KUUA ABIRIA SITA |
Tukio hilo lilitokea jana saa 4:00 asubuhi katika ajali iliyohusisha basi dogo la abiria aina ya Toyota Hiace lililokuwa likitokea
mjini Mbeya kwenda Chimala wilayani Mbarali na lori aina ya FAW
lenye tela lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda
nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Katika ajali hiyo, watu watano walifariki papohapo na mmoja
alifariki akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya
alikopelekwa kupatiwa huduma.
| BAADHI YA MAJERUHI WAKIFIKISHWA KATIKA HOSPITALI YA RUFAA MBEYA. |
Akithibitisha kupokea
miili ya marehemu na majeruhi hao, Ofisa
Muuguzi wa Kitengo cha Huduma za
Dharura, Jenny Kapeye alisema kuwa alipokea miili ya marehemu watano
waliofariki eneo la tukio na mmoja alifariki akiwa anapatiwa huduma hospitalini
hapo.
Aliwataja waliopoteza maisha katika ajali hiyo kuwa ni
Steven Kimario, Shalfa Abdallah, Simon
Mwakalikwa, Andrew Simbeye, Mariam Mwanginde
na mwanamume mwingine ambaye hakufahamika jina lake mara moja.
Miili yote imehifadhiwa katika hospitali hiyo ya rufaa.
Majeruhi waliofikishwa hospitalini hapo ni 10 na kati yao
saba walitibiwa na kuruhusiwa huku watatu ambao ni Elia Malowe, Charles Gumani
na Doto Tagala wamelazwa wodini.
Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Diwani Athumani
alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo ambapo alisema kuwa uchunguzi wa awali
ulibaini kwamba dereva wa lori hilo
alikuwa akiendesha gari huku akiwa amelewa pombe aina ya Konyagi.
Kwa mujibu wa Kamanda Athumani, pombe hiyo ilikutwa ndani ya
gari hilo na wananchi waliofika kutoa msaada na baada ya kugundua hilo ulizuka
mgogoro mkubwa uliosababisha dereva huyo kutaka kupigana na wananchi hao.
Kamanda Athumani alisema Jeshi la Polisi linamshikilia
dereva huyo kwa uchunguzi zaidi.
Ajali hiyo imekuja ikiwa ni siku 40 tangu kutokea ajali
nyingine mkoani humo iliyosababisha watu 10 kufariki dunia na wengine 25
kujeruhiwa akiwamo Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Mery Mwanjelwa baada ya lori
la mafuta kushindwa kufunga breki na
kuyagonga magari mengine matatu katika mteremko wa Mlima wa Iwambi – Mbalizi
nje kidogo ya Jiji la Mbeya.
Picha na LUKAZA BLOG.
No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA