MAONYESHO YA ASILI DAR ES SALAAM, MAANDALIZI YAKE YAKAMILIKA: ASILI YETU BLOG
Asili Yetu © All rights reserved
Maandalizi ya MAONYESHO YA ASALI YA DAR ES SALAAM (DAR ES
SALAAM HONEY EXHIBITION) ambayo yatafanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere
(Sabasaba) Dar es Salaam tangu tarehe 3 hadi 7 Oktoba 2012 yamekamilika.
Wananchi wanakaribishwa kuhudhuria maonyesho hayo ambayo hayatakuwa na
kiingilio.
Katika maonyesho hayo watu wataelimika kuhusu manufaa
yatokanayo na asali, pia watapata utaalam wa kufuga nyuki na wataonja na
kununua asali bora kwa bei nafuu. Kaulimbiu ya maonyesho hayo ambayo ni ya
kitaifa ni ASALI KWA AFYA NA USTAWI (HONEY FOR HEALTH AND PROSPERITY).
Maonyesho hayo yameandaliwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Maliasili na Utalii,
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) na wadau
wengine wa Sekta ya Ufugaji Nyuki. Lengo kuu la maonesho ni kuhakikisha
upatikanaji wa masoko ya uhakika ya mazao ya nyuki. Tarehe 3 Oktoba ni siku
iliyotengwa maalum kwa ajili ya kufanyika Kongamano la Ufugaji Nyuki. Hivyo
wafugaji nyuki, wataalam na wadau mbalimbali wa Sekta hiyo wanakaribishwa
kuhudhuria kungamano hilo
ambalo litafanyika katika ukumbi wa J. M. Kikwete ulioko kwenye viwanja vya
Mwalimu Nyerere .
Ufunguzi rasmi wa maonyesho hayo utafanyika tarehe 5 Oktoba
2012 ambapo Mgeni Rasmi anategemewa kuwa Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Mizengo Peter Pinda (Mb). Waonyeshaji waliothibitisha kushiriki
ni Halmashauri za Wilaya zote, kampuni zinazonunua asali, watengenezaji wa
mizinga na vifaa vingine vya kisasa vya ufugaji nyuki, na watengenezaji wa
bidhaa zinaotumia asali na nta kama malighafi.
Inategemewa kuwa katika maonyesho hayo waonyeshaji watajitangaza ili waweze
kupata wanunuzi wa asali na mazao mengine ya nyuki.
Pia wanunuzi wa mazao ya nyuki watapata fursa ya kuwafahamu
wafugaji. Aidha inategemewa kuwa utaundwa mtandao ambao utawaunganisha
wazalishaji, wafanyabiashara, wataalam na wadau wa sekta ya nyuki.
George Matiko
MSEMAJI WIZARA YA
MALIASILI NA UTALII
30 Septemba 2012
Simu: +255 784 468047

No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA