ZIARA YA RAIS JAKAYA KIKWETE YA MAREKANI NA CANADA YAANZA LEO: ASILI YETU BLOG
Asili Yetu © All rights reserved
THE UNITED REPUBLIC
OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: ikulumawasiliano@yahoo.com
press@ikulu.go.tz
Fax: 255-22-2113425
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete anaanza Ziara ya Kikazi ya Marekani na Ziara Rasmi ya Kiserikali
ya Canada akianzia mjini New York, Marekani leo, Jumatatu, Oktoba Mosi, 2012.
Rais Kikwete na ujumbe wake uliondoka nchini usiku wa jana,
Jumapili, Septemba 30, 2012, na utawasili mjini New York, Marekani mchana wa
leo tayari kwa ziara hiyo ya Marekani.
Rais Kikwete atakuwa Marekani kwa siku mbili kabla ya kwenda
Canada kwa ziara Rasmi ya Kiserikali ya siku mbili.Katika ziara yake mjini New
York, Marekani, Rais Kikwete atakutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa Mheshimiwa Ban Ki Moon ofisini kwa Katibu Mkuu huyo kesho
asubuhi Oktoba 2, 2012.
Baada ya mazungumzo hayo, Rais Kikwete ataungana na
Mheshimiwa Ban Ki Moon, Meya wa Jiji la New York na Mfadhili Mkubwa wa Misaada
ya Kibinadamu Duniani, Mheshimiwa Michael Bloomberg; Mama Helen Agerup ambaye
ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Misaada ya Kibinadamu ya H&B Agerup na Dkt.
Kelly J. Henning, Mkurugenzi wa Mipango ya Sekta ya Afya ya Taasisi ya
Bloomberg Philanthropies kwenye Uzinduzi wa Matokeo ya Mpango ya Ubunifu wa
Afya ya Akinamama katika Tanzania.
Kwenye sherehe hiyo iliyopangwa kufanyika kwenye ukumbi
uitwao Green Room kwenye makao makuu wa Umoja wa Mataifa, Rais Kikwete,
Mheshimiwa Ban Ki Moon, Meya Bloomberg na mama Helen Agerup kwa pamoja
watazindua Matokeo ya Mpango huu uitwao Innovative Maternal Health Program.
Kwenye shughuli hiyo pia Meya Bloomberg atatangaza matokeo
ya miaka mitatu ya misaada ya kiafya chini ya mpango huo kwa akinamama
iliyotolewa na taasisi ya inayomilikiwa na Meya Bloomberg ya Bloomberg
Philanthropies. Aidha, kwenye shughuli hiyo, Meya Bloomberg atatangaza misaada
mpya wa mabilioni ya fedha kuboresha afya ya akinamama katika Tanzania chini ya
mpango huo na atatangaza mshirika mpya ambaye atasaidiana na taasisi ya
Bloomberg Philanthropies katika kuunga mkono huduma bora za afya kwa akinamama
wa Tanzania.
Katika Tanzania, misaada ya taasisi ya Bloomberg
Philanthropies huelekezwa katika maeneo ya vijijini yasiyokuwa na huduma bora
zaidi kwa kiafya na huduma ambazo hutolewa ni zile za kuokoa maisha ya akina
mama hasa wakati wa uzazi.
Tokea mwaka 2006, taasisi hiyo imetoa kiasi cha dola za
Marekani milioni 11.5 Fedha hizo ni sehemu ya kiasi cha dola za Marekani
milioni 330 ambazo zilitolewa na taasisi hiyo kwa nchi mbali mbali duniani kwa
mwaka jana peke yake.
Taasisi hiyo hufanya kazi ya kuendeleza maeneo matano
duniani ambayo ni Usanii, Elimu, Mazingira, Ubunifu katika Serikali na Afya ya
Umma.Rais Kikwete ataondoka Marekani kwenda Canada keshokutwa Jumatano Oktoba
3, 2012 kwa ajili ya Ziara Rasmi ya Kiserikali ya siku mbili katika nchi hiyo
kwa mwaliko wa Gavana Jenerali wa nchi hiyo, Mheshimiwa David Johnston.
No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA