MKUTANO WA MAPINDUZI YA KIJANI AFRIKA (AGRA) KUFANYIKA ARUSHA MWEZI HUU.
Asili Yetu © All rights reserved
Rais wa AGRA Bi. Jane Kaluku (katikati) akifuatiwa na Mkurugenzi wa mfuko wa AGRA Bi. Anne Mbaabu (kushoto) na mwisho ni muwakirishi wa AGRA nchini Bwana.Fredy Muhhuku wakiwa wanazungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano huo utakao anza mwezi huu.
Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa jukwaa la mapinduzi ya kijani Afrika utakaofanyika kuanzia Septemba 26 hadi Septemba 28 mjini Arusha. Mkutano huo utawakutanisha viongozi mbali mbali wa kimataifa ambao watajadili namna ya kuchukua hatua katika kuboresha usalama wa chakula duniani.
Aidha katika mkutano huo viongozi hao wataweza kujadili sera ya mapinduzi ya kilimo na uchumi wa
Afrika ,njia za kukuza masoko pamoja na namna ya kubadilisha mfumo wa kilimo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa Rais wa umoja
wa mapinduzi ya kijani Afrika (AGRA) bi Jane
Karuku alisema kuwa mkutano huo
ni hatua inayofuata katika kuendeleza bara
la Afrika kupata ufumbuzi katika masuala ya usalama wa chakula.
Karuku alisema kuwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo
katika kukuza sekta ya ukuaji wa kilimo inawakilisha uchunguzi uliofanywa katika wilaya ya kilombero mkoa wa
morogoro juu ya njia bora za kilimo.
Alieleza kuwa uchunguzi huo uliwezesha uzalishaji wa mahindi
kwa wakulima wadogo wa wilaya hiyo kuongezeka kutoka tani 1.5 hadi 4.5 kwa
hekta ,ambapo kwa upande wa mavuno ya mpunga yaliongezeka kutoka tani 2.5 hadi
tani 6 hali iliyopelekea Tanzania kupata
fursa hii ya kuwa mwenyeji wa mkutano
huo.
Aidha alisema kuwa jukwaa hilo litatoa nafasi ya kujadili
namna bora ya kuendeleza mipango ya uwekezaji wenye tija kwa ajili ya
kuongeza maendeleo ya kilimo barani
Afrika pamoja na kujadili namna bora ya kuunganisha nguvu ya jamii na sekta
binafsi katika kuboresha usalama wa chakula duniani
Aliongeza kuwa jukwaa hilo pia litaweza kujadili na kutafuta
njia bora za kuboresha kilimo barani Afrika na kuwawezesha wakulima wadogo
wadogo kushirikiana na vyama vya
ushirika na wadau wengine ambapo mjadala huo utatoa njia bora za matumizi ya
rasilimali na kukabiliana na changamoto zinazowakabili mamilioni ya wakulima barani Afrika.
“Wakulima wadogo wadogo ni kitovu kwa yale yote tuyafanyayo
hivyo mtazamo wetu ni kuwapatia wakulima wa afrika dhana za kilimo wanazohitaji
ili waweze kukua zaidi na kuongeza kipato chao na watatuongoza katika kupata
mafanikio mazuri”Alisema bi Jane

No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA