AIRTEL TANZANIA YAKABIDHI SHILINGI MILIONI 5 NA T SHIRT 400 KWAAJILI YA MASHINDANO YA RIADHA YA ROCK CITY.
Asili Yetu © All rights reserved
Ofisa Uhusiano wa kampuni ya Airtel Tanzania, Bi Jane
Matinde (kulia) akimkabidhi hundi ya shilingi milioni tano Meneja Matukio wa
kampuni ya Capital Plus International ambaye pia ni Mratibu wa mbio za Rock
City Marathon za mwaka huu, Bi Grace Sanga jijini Dar es Salaam jana kama
sehemu ya udhamini wa mbio hizo zitakazofanyika katika uwanja wa CCM Kirumba
jijini Mwanza tarehe 28 Oktoba. Airtel pia walikabidhi T-shirt mia nne
zitakazotumika katika mbio hizo.
KAMPUNI ya mawasiliano nchini ya Airtel imeahidi kuendelea
kusaidia michezo mbalimbali nchini ikiwa na lengo la kukuza maendeleo ya
vijana.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana katika hafla fupi ya
kukabidhi shilingi milioni tano pamoja na T-shirt mia nne kama udhamini wa mbio
za Rock City Marathon za mwaka huu zenye kauli mbiu ‘tukuze utalii wa ndani
kupitia michezo’, Afisa Uhusiano wa Airtel, Bi Jane Matinde alisema kuwa
kampuni yake itaendelea kusaidia michezo mbalimbali nchini ikiwemo riadha ili
kukuza maendeleo ya vijana.
“Udhamini wetu wa shilingi milioni tano pamoja na T-shirt
mia nne katika mbio za Rock City mwaka huu unalenga katika kusukuma maendeleo
ya vijana kupitia michezo kwa kuwa tunaamini kuwa michezo imekuwa ni chanzo
kikubwa cha ajira duniani.
“Tunaahidi kuendelea kusaidia michezo mingine kwa kuwa pia
tunaamini kupitia michezo mbalimbali tunaweza kutangaza vivutio vyetu vya
utalii duniani. Mfano nzuri ni mbio za mwaka huu za Rock City Marathon
zitakazowakutanisha wanariadha mbalimbali kutoka nchi jirani,” aliongeza Bi.
Matinde.
Akipokea hundi na T-shirt hizo, Mratibu wa mbio hizo kutoka
katika kampuni ya Capital Plus International (CPI), Bi. Grace Sanga aliishukuru
kampuni ya Airtel kwa kuendelea kusaidia mbio za Rock City na kuyahasa
mashirikia na makampuni mengine kuiga mfano wa kampuni hiyo.
“Tunaishukuru Airtel kwa msaada wao kwa kuwa msaada huu
utatusaidia tujiandae vizuri na Rock City Marathon ya mwaka huu itakayofanyika
Oktoba tarehe 28 katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza,” alisema Grace.
Grace alisema kuwa mbali na Airtel wadhamini wengine ni
pamoja na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Parastal Pension Fund (PPF),
Geita Gold Mine, African Barrick Gold, Air Tanzania Company Ltd (ATCL), Mamlaka
ya Taifa ya Mbuga za Wanyama nchini (TANAPA), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB),
Nyanza Bottles, New Africa Hotel na New Mwanza Hotel.
Aidha, Bi Sanga aliwaasa wanariadha kujitokeza na kuanza
kujisajili ili kushiriki katika mbio hizo na kusema kuwa fomu za usajili
zinapatikana katika ofisi za uwanja wa CCM Kirumba, ofisi za kampuni ya Capital
Plus International zilizopo katika jengo la ATCL ghorofa ya tatu, ofisi za Bodi
ya Utalii jengo la IPS ghorofa ya tatu, Dar es Salaam, na zinapatikana katika
tovuti ya www.rockcitymarathon.blogspot.com.
CPI ilitangaza kuwa atakayeibuka kinara katika mbio za
kilometa 21 mwaka huu kwa wanaume na wanawake atazawadiwa shilingi milioni moja
na laki mbili wakati mshindi wa pili ataweka mfukoni shilingi laki tisa na
mshindi wa tatu ataondoka na shilingi laki saba.

No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA