RAIS KIKWETE AONGOZA WAOMBOLEZAJI KUAGA MIILI SABA YA WANAJESHI WALIOUAWA SUDANI. (ITV HABARI)
Amirjeshi mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama Rais Jakaya Kikwete
akiongozana na viongozi mbalimbali waandamizi katika serikali ya jamhuri
ya muungano na serikali ya mapinduzi ya Zanzibar na watu maarufu
amewaongoza mamia ya waombolezaji katika kuiaga miili saba ya wanajeshi
wa jeshi la wananchi wa Tanzania waliouwawa nchini Sudan Jumamosi ya
July 13 mwaka huu.
Dr Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza katika viwanja vya makao makuu
ya jeshi hilo akionekana dhahiri shairi mwenye majonzi ikiwa ni muda
mfupi mara baada ya kuwaongoza mamia ya waombolezaji kuiaga miili ya
wanajeshi hao waliouwawa na kikundi cha waasi nchini Sudan katika jimbo
la Darfur amesema taarifa za tukio hilo limemuhuzunisha,kumsikitisha na
kumkasirisha na kushauri kuwa wakati umefika wa kuutazama upya mfumo
mzima wa kulinda amani Darfur hasa kuhusu kiwango cha uwezo wa wanajeshi
kujilinda kutokana na ukweli kuwa tayari walinda amani 41 kutoka
mataifa mbalimbali wameuwawa na wengine 55 kujeruhiwa.
Aidha waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga taifa Mh Shamsi Vuai
Nahodha amekiita kitendo cha wanajeshi hao wakulinda amani kuuwawa ni
dhahiri tendo ovu ambao ni mkakati maalum wa waasi kutaka kuhakikisha
mpango wa umoja wa mataifa katika kuleta amani katika nchi zenye
mifarakano hazifanikiwi huku salamu za rais wa mapinduzi ya Zanzibar Dr
Ally Mohamed Shein zikisomwa na mwakilishi.
Mkuu wa majeshi ya ulinzi hapa nchini jenerali Davis Mwamunyange
amesema wanajeshi hao walishambuliwa na waasi wakati wakisindikiza na
kutoa ulinzi kwa waangalizi wa amani na washauri wa polisi na kwamba
walipopunguza mwendo kutokana na utelezi uliosababishwa na mvua umbali
wa kilomita 25 kutoka Darfur ndipo waliposhambuliwa.
Zoezi hilo la kuiaga miili ya mashujaa hao waliouwawa nchini Sudan
mbali na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali waandamizi serikalini pia
limehudhuriwa na watu mbalimbali maarufu akiwemo mwenyekiti mtendaji wa
makampuni ya IPP Dr Regnald Mengi huku aliyekuwa naibu katibu mkuu wa
umoja wa mataifa Dr Asha Rose Migiro akisema tukio hilo lisiwakatishe
tamaa katika kupigania amani ya watu wengine katika nchi zenye
mifarakano.
Source: ITV TANZANIA
No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA