RAIS WA VENEZUELA HUGO CHAVEZ AFARIKI DUNIA.
![]() |
Aliyekuwa rais wa Venezuela Hugo Chavez enzi za uhai wake. |
Katika taarifa kwa taifa, makamu wa rais wa
Venezuela Nicholas Marduro ametangaza kufariki dunia kwa rais Hugo
Chavez, 58, kufuatia kuugua muda mrefu maradhi ya Saratani. Rais Chavez
ametoweka katika hadhira ya nchi hiyo kwa muda mrefu ambapo alikuwa
anapokea matibabu nchi jirani ya Cuba.
Taarifa kutoka kwa jeshi imesema kuwa wataendelea kuilinda hadhi ya nchi na kuimarisha usalama. Pia jeshi limeahidi kuendelea kuwa waaminifu kwa makamu wa rais Nicholas Marduro na wakatoa wito kwa raia kuwa watulivu.
Chavez - wasifu
Hugo Chavez alijitosa katika siasa za Venezuela mnamo Februari 1992 akiwa luteni katika jeshi. Aliongoza mapinduzi dhidi ya rais wa wakati huo Carlos Andres Perez.
Lakini kutokana na kukosa usaidizi wa kutosha wa kijeshi, Chavez na wanamgambo wenzake walishindwa kunyakua madaraka hayo. Alikiri kushindwa na aliwekwa korokoroni.
Aliingia uongozini baada ya ushindi mkubwa ulioviondosha vyama vya kisiasa wakati huo. Katika kuapishwa kwake mnamo February 1999, Hugo Chavez alitangaza wazi kwamba mipango yake ya mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi sio kampeni tu. Alitimiza ahadi yake na kuiongoza nchi hiyo katika mabadiliko ambayo hayakuwahi kushuhudiwa katika muda wa miongo kadhaa. Alibadili muundo wa bunge na kulifanya kuwa la kikatiba, ambalo liliiunda katiba mpya baada ya kura ya maoni iliyoidhinishwa na 88% ya wapiga kura.
Rais Chavez alitaifisha rasilmali ukiwemo utajiri wake mkubwa wa mafuta. Sera kama hizi zilimfanya azozane na kampuni za kimataifa za mafuta, lakini alipata uungwaji mkono mkubwa wa watu maskini.
Chavez na jamii ya kimataifa
Kutokana na urafiki wake na viongozi wa mrengo wa kushoto kama vile rais wa Cuba, Fidel Castro, ambaye walikuwa na uhusiano wa karibu aligongana kidiplomasia na Marekani, ambayo ni mshirika wake mkuu wa kibiashara.
Chavez alipendwa nyumbani na wafuasi wake lakini alipingwa na baadhi ya watu nchini humo na katika nchi za nje. Alionekana sio tu kama bingwa wa jamii maskini lakini pia kama muingiliaji wa siasa za nchi jirani. Katika miaka ya hivi karibuni alilenga kukabiliana na masuala ya ndani ya Venezuela, kama uhalifu, kuinua uchumi wa nchi na kukabiliana na rushwa.
Chanzo cha habari hii ni BBC SWAHILI
No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA