TUTAPUNGUZA BEI YA UMEME VIWANDANI - DK KIGODA.
![]() |
Dk. Kigoda |
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda amesema
atapambana kuhakikisha viwanda vinapunguziwa bei ya umeme ili kuleta ufanisi wa
uzalishaJi wa bidhaa.
Amesema hayo wakati Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco)
tayari limewasilisha kwa Mamlaka ya Kudhibiti Huduma za Nishati na Maji (Ewura)
maombi ya kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 150 ifikapo Januari mwakani.
Akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Shirika la Wenye
Viwanda Tanzania (CTI), jijini Dar es Salaam jana, Dk Kigoda alisema kwa
kushirikiana na wataalamu mbalimbali wataangalia tozo za gharama za umeme kwa
viwanda nchini.
Alisema mpango huo wa kupunguza gharama za umeme zinalenga
kuviwezesha viwanda kuzalisha kiwango cha juu ukilinganisha na sasa.
“Viwanda vinaweza kufanya vizuri endapo nishati hiyo
itapatikana kwa uhakika kwani bila hivyo itakuwa ngumu kuzalisha bidhaa nyingi
na bora,” alisema Dk Kigoda na kuongeza:
“Mfano unaangalia katika kiwanda kimoja, asilimia 40 ya
mapato wanatumia kulipia gharama ya umeme, lakini ikiwa watatumia asilimia 20
kiwanda kitazalisha kwa urahisi na bei itapungua,” alisema.
Dk Kigoda alisema suala la bidhaa zisizo na ubora hapa
nchini limeendelea kushamiri na hivi sasa limefikia asilimia 20 ya bidhaa zote
zinazouzwa sokoni.
“Ninyi CTI mtakuwa mnawajua wafanyabiashara wanaiongiza
bidhaa bandia hivyo tunaomba muwataje ili waweze kuchukuliwa hatua sitahiki,”
alilalamika Dk Kigoda.
Naye, Mwwenyikiti wa CTI, Felix Mosha alisema suala la
bidhaa bandia kuwepo sokoni linatokana na Serikali kutokutekeleza kwa vitendo
ukaguzi wa bidhaa kabla hazijaingia nchini.
“Serikali inatakiwa kutekeleza kwa vitendo ukaguzi wa bidhaa
kabla hazijaingia nchini. Hii itasaidia kuhakikisha haziingii katika masoko,”
alisema Mosha.
No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA