ASKOFU MALASUSA AIKOMALIA SERIKALI KUHUSU WALIOCHOMA MAKANISA.
WAKATI baadhi ya vinara wa vurugu zinazohusishwa na masuala
ya kidini wakiwa Mahakamani jijini Dar es Salaam na Zanzibar, Mkuu wa Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri (KKKT) na Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk
Alex Malasusa ameidai kuwa Serikali ina kigugumizi katika kusema ukweli
kuhusiana na vurugu hizo na zingine zinazotokana na imani za kidini nchini.
Akihutubia wakati wa kufungua Mkutano Mkuu wa 31 wa Dayosisi
ya Mashariki na Pwani unaofanyika mjini Bagamoyo jana, Askofu Malasusa alisema
kuwa, Serikali ilipaswa si tu
kuwakamata, bali pia kufuta usajili wa vikundi vyote vinavyosababisha vurugu
nchini.
Askofu Malasusa alisema kuwa, kitendo cha Serikali kukaa kimya bila kuchukulia hatua
vikundi vilivyosajiliwa na kuwa na mlengo tofauti na madhumuni yake ama
inapendezwa, kuvutiwa na hata kushawishiwa na yale ambayo yanazungumzwa na
vikundi hivyo japo wanaweza wasikubaliane na vitendo vyao.
Kuanzia katikati ya Oktoba mwaka huu, kulizuka ghasia katika
mji wa Zanzibar
na vitongoji vyake zinazodaiwa kufanywa na wafuasi wa Kikundi cha Uamsho
vilivyokwenda sambamba na kuchoma makanisa.
Katika mfululizo wa matukio hayo, makanisa takriban saba
yalichomwa moto jijini Dar es Salaam
baada ya kuzuka ghasia maeneo ya Mbagala, wilayani Temeke, zilizotokana na
imani za kidini na watu 49 walikamatwa na baadaye kuachiwa huru.
Hata hivyo, kesi bado ziko mahakamani kwa viongozi wa
wafuasi hao ambao kwa Zanzibar ni Farid Hadi
Ahmed na Dar es Salaam,
Sheikh Ponda Issa Ponda.
“Naomba serikali ipige marufuku vikundi hivi, hatutaki
viendelee wala kupewa nafasi kushamiri hata kama ni ndani ya kanisa
ninaloliongoza kwani yaliyotokea Rwanda
na Burundi na hata Kenya. hatutaki
yatokee hapa kwetu” alisema Askofu Malasusa.
Mkuu huyo wa Kanisa alisema katika hotuba yake ya ufunguzi
kuwa, pamoja Wakristo wamejifunza kupitia maandiko Matakatifu kuwa: ‘Kushindana
kwetu sio kwa juu ya damu na nyama bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya
wakuu wa giza hili, majeshi, pepo wabaya katika ulimwengu wa roho’, hana
uhakika kama wote wana uvumilivu wa kutosha.
“Sina hakika mtu akija na silaha kushambulia na wewe upo ndani na silaha na biblia kama
utatoka na biblia, au silaha,” alisema Mkuu huyo wa KKKT na kusisitiza kuwa,
jambo ambalo halitakiwi litokee nchini.
Askofu Malasusa alitoa wito kwa serikali kushirikiana na
taasisi za dini kikamilifu kudumisha umoja, amani na mshikamano wa kindugu
miongoni mwa Watanzania.
“Tumeshuhudia uchomaji wa makanisa huko Zanzibar, Mwanza,
Mdaula, Mto wa Mbu, Tunduru, Rufiji, Kigoma na hapa Dar es Salaam, vitendo
ambavyo si utamaduni wa Watanzania ambako kwa asili ni wamoja, wanapendana sana
wanashirikiana bila kujali tofauti ya dini zao,” alisema Malasusa na kuongeza;
“Watanzania wengi wanasikitishwa sana
vikundi vinavyochochea chuki na uhasama baina yao, hivyo Serikali inatakiwa kuchukua hatua
zinazotakiwa kwa mujibu wa sheria za nchi vinginevyo amani ya nchi yetu itakuwa
mashakani.”
Malasusa ambaye alisema kuwa, ingawa Tanzania
inatajwa kuwa kisiwa cha amani, matukio yaliyotokea hivi karibuni yanatia shaka.
Alisema kitendo cha kuchomwa moto makanisa na watu
wanaodaiwa kuwa ni Waislamu wenye msimamo mkali
kilimuogopesha sana kwani lingeweza
kutokea lolote kama upande wa pili wangeamua
kulipiza kisasi.
Source:Mwananchi
No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA