WATOTO WILAYANI KARAGWE MKOANI KAGERA, WARIPUKIWA BOMU NA KUFARIKI.
Asili Yetu Tanzania.Copyright
Watoto watano ,watatu wakiwa wa familia moja wamekufa
Wilayani Karagwe mkoani Kagera Magharibi mwa Tanzania.
Ni baada ya kulipukiwa na bomu la kutupwa kwa mkono wakati
walipokuwa wakichezea Bomu hilo lililookotwa kwenye vyuma chakavu na kudhani
kuwa ni mpira.
Tukio hilo lilitokea Jumatano majira ya asubuhi huko
Wilayani Karagwe mkoani Kagera Magharibi mwa Tanzania wakati watoto walipokuwa
wakichezea kitu mfano wa mpira mdogo ,ambacho baadaye kilikuja kutambulika kuwa
lilikuwa Bomu la kurushwa kwa mkono.
Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC mjini Dar es Salama, Eric
David Nampesya, mkuu wa Wilaya wa Karagwe Bi Darli Rwegasira amesema kuwa
watoto hao walilipukiwa na Bomu hilo ambapo watatu kati yao walikufa papo hapo
huku wawili wakifia hospitalini.
Kwa Mujibu wa Mkuu huyo wa Wilaya, awali mzazi wa watoto hao
amekiri kuwa aliliona bomu nyumbani kwake hapo juzi ambapo watoto wake walikuja
nalo baada ya kuliokota huku wakidhani kuwa ni mpira.
Naye Kamanda wa Polisi mkoani Kagera Philipo Kalangi alisema
kuwa utafiti waliofanya umeonyesha kuwa Bomu hilo lililookotwa na kijana mmoja
ambaye alikuwa akikusanya vyuma chakavu kwa lengo la kuviuza hapo wilayani
karagwe.
Bomu hilo lilikuwa mojawapo katika vyuma alivyokuwa ameokota
na baadaye watoto hao walienda kulichezea nyumbani kwao na hatimaye kusababisha
maafa hayo.
Mkuu huyo wa Polisi mkoani Kagera alidokeza kuwa uchunguzi
unaendelea ili kujua kwa undani Bomu hilo lilitokea wapi na iwapo kama kuna
mabomu mengine yanayoweza kuwa yamebaki katika maeneo mbali mbali hapo Wilayani
Karagwe.
Mkuu huyo wa Polisi hakuweza kukiri wala kukana moja kwa
moja kuhusisha Bomu hilo Kama matokeo ya uwepo wa wakimbizi wa Rwanda waliowahi
kuishi Wilayani hapo mwaka 1994 baada ya mauaji ya kimbari nchini Rwanda ambapo
Wilaya ya Karagwe ni moja ya wilaya zilizopokea wakimbizi wengi kutoka nchini
Rwanda.
Uchunguzi zaidi unaendelea huku ukiwahusisha wataalam wa
milipuko kutoka Polisi na jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.
No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA