POLISI WAJERUHI KWA MABOMU DAR, RUFIJI.
POLISI wamewajeruhi watu watatu kwa mabomu, mmoja kati yao akiwa katika hali mbaya katika matukio mawili tofauti
ya kusambaratisha mikusanyiko iliyotokea Tegeta, Dar es Salaam na Rufiji mkoani Pwani.
Aliyejeruhiwa vibaya ametambuliwa kuwa mkazi wa Tegeta, John
Paul ambaye baada ya tukio hilo
alipelekwa katika Hospitali ya Mwananyamala na baadaye Muhimbili.
Tukio la Tegeta lilitokea wakati polisi walipokuwa
wakiwatawanya wananchi waliokuwa wakipinga operesheni ya kuwaondoa katika
hifadhi ya barabara katika eneo hilo saa nne
asubuhi baada ya wafanyakazi wa Kampuni ya Udalali ya Mwankinga wakiwa na
polisi waliyolikamata gari la mkazi mmoja wa eneo hilo.
Hali hiyo ilizua ubishi na baadaye vurugu baada ya wakazi
hao kutaka gari hilo
lisichukuliwe na polisi.
Vurugu hizo ziliwafanya polisi kutumia nguvu kuwatawanya
wakazi hao, kazi ambayo hata hivyo, haikuwa rahisi kwani nao walikuwa wakijibu
kwa kuwarushia mawe na fimbo, hali iliyodumu kwa saa kadhaa na kufanya eneo hilo kugeuka uwanja wa mapambano kusababisha maduka
kufungwa na mali
kuharibiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Chales Kenyela
alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo na kueleza kuwa, kijana huyo alijeruhiwa
shavuni na kitu ambacho bado hakijafahamika na kupelekwa katika Hospitali ya
Mwananyamala kwa matibabu.
Kamanda Kenyela alisema kuwa, polisi bado wanaendelea na
uchunguzi wa tukio hilo
na taarifa zaidi zitatolewa baadaye. Alisema awali, wafanyakazi wa kampuni hiyo
wakiwa na polisi, walifika eneo hilo
na kuanza operesheni ya kuondoa magari.
“Walipokamata gari la mmoja wa wakazi wa eneo hilo wananchi hao
walipinga na kuanza kuwafanyia vurugu polisi ambao walijibu mapigo kwa kupiga
mabomu ya machozi na kuwatawanya. Kijana huyo alionekana baadaye akiwa
amejeruhiwa na kupelekwa Mwananyamala,” alisema. Katibu wa Afya katika
Hospitali ya Mwananyamala, Edwin Bisakala alithibitisha kupokewa kwa majeruhi
huyo na kudai kuwa uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa alijeruhiwa kwa bomu.
Bisakala alisema hali ya majeruhi huyo ilikuwa mbaya na
uongozi wa hospitali ulilazimika kumpeleka Muhimbili kwa uchunguzi na matibabu
zaidi.
Mmoja wa mashuhuda wa vurugu hizo ambaye hakutaka kutaja
jina lake alisimulia
jinsi eneo hilo
lilivyokuwa: “Polisi wanarusha mabomu na wananchi wanawarushia mawe, ilikuwa
tafrani kubwa hapa.”
Alisema hali hiyo iliwafanya polisi wajibu kwa kupiga risasi
hewani na kufyatua mabomu ya machozi hali iliyozua taharuki na baada ya watu
kutawanyika, kijana huyo alionekana akiwa ameanguka chini, huku damu zikimvuja.
Ofisa Habari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel
Eligaeshi alithibitisha kufikishwa kwa kijana huyo katika hospitali hiyo
akimtaja kwa jina la John Massawe. Alisema alikuwa amejeruhiwa vibaya kichwani.
Mabomu 22 Rufiji
Wilayani Rufiji, polisi walitumia mabomu 22 ya machozi
kuwatawanya wananchi wa Kijiji cha Mgomba Kati waliozingira jengo la kufua
umeme wakipinga hatua ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kuondoa mashine
mbili za kufua umeme bila wao kuwa na taarifa na kuzipeleka wilayani Liwale,
Mkoa wa Lindi.
Mwandishi wa habari aliyekuwapo eneo la tukio saa nne
asubuhi alishuhudia umati mkubwa wa watu wakiwa katika eneo hilo wakipinga kuondolewa kwa mashine hizo.
Wananchi hao walisema licha ya kuwa na umeme unaotumia gesi
ya Songosongo, jenereta hizo huwasaidia wakati umeme huo wa gesi unapokosekana
huku wakisema hawakushirikishwa katika uhamishwaji huo.
Askari wawili walifika katika eneo la tukio na kuwaamuru wananchi
hao kuondoka katika eneo hilo
bila mafanikio. Baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya, polisi hao walikimbia
huku wananchi wakiwa na mawe wakiwafukuza. Askari mmoja aliyekuwa na bomu la
machozi alidandia pikipiki na kukimbia na kumuacha mwenzake ambaye
alishambuliwa vibaya kwa mawe.
Askari huyo aliyeachwa aliepuka kipigo baada ya kukimbilia
katika nyumba moja ya msamaria mwema na kujificha.
Baadaye polisi wenye silaha waliwasili eneo la tukio na
kuanza kufyatua mabomu mfululizo kuwasambaratisha wananchi hao waliokuwa
wamelizunguka jengo hilo
wakitaka gari ambalo linasadikiwa kuwa lilikodiwa kwa ajili kunyanyua mashine
hizo liondoke.
Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Ikwiriri, Dk Idi Malinda
alisema raia wawili na polisi mmoja aliyetambulika kwa jina la Ali walifikishwa
hapo kwa matibabu baada ya vurugu hizo.
Aliwataja raia waliofikishwa hapo kuwa ni Seif Baja ambaye
alijeruhiwa mkono wa kushoto, Hemedi Juma aliyeumia kichwani na askari Ali
ambaye aliumia sehemu mbalimbali za mwili. Wakati hayo yakitokea katika eneo la
tukio, wananchi wengine katikati ya Mji wa Ikwiriri walifunga Barabara Kuu ya
Kibiti kwenda Lindi kwa zaidi ya saa moja na kusababisha usumbufu mkubwa kwa
abiria waliokuwa wanatumia njia hiyo.
Hali ilitulia ilipofika saa 8:46 mchana baada ya polisi
kuongeza nguvu kukabiliana na wananchi hao. Meneja wa Tanesco Tawi la Ikwiriri,
Ladslaus Kalisa alisema mashine hizo mbili zilikuwa zikipelekwa Liwale kwa kuwa
Ikwiriri ilipoanza kutumia umeme wa gesi, mashine hizo hazifanyi kazi.
Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Nurdin Babu alilaani tukio hilo akisema Serikali
iliamua kuzipeleka mashine hizo Liwale kwa nia njema ya kuwasaidia wananchi
wenzao ambao wanakabiliwa na shida ya umeme.Babu aliwataka wananchi wa Ikwiriri
kufuata taratibu za kisheria kudai kile wanachoamini akisema Wilaya ya Rufiji
kuonekana kila mara kuwa chanzo cha matatizo siyo sifa njema.
Alisema mashine hizo haziendi kuuzwa kama ambavyo wananchi
hao wanadai bali zinakwenda Liwale kuwasaidia watanzania kama
wa Ikwiriri ambao kwa sasa wanauhakika wa Umeme wa gesi.
Sorce:Mwananchi
No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA