MZEE MAKAMBA ATIKISA, AKEMEA KURA ZA MARUHANI KWA JK.
Mzee Yusufu Makamba
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) jana kimenusuru Rais Jakaya
Kikwete kupigiwa kura za maruhani, baada ya kubadili taratibu za uchaguzi, huku
Katibu Mkuu wake wa zamani, Yusuph Makamba akiwapiga vijembe waliokuwa
wamepanga mbinu hizo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa CCM, Spika wa Bunge,
Anne Makinda, muda mfupi kabla wajumbe hawajaanza kupiga kura alitangaza
utaratibu mpya kwamba kila mkoa utapiga kura katika sanduku lake.
“Kila mkoa utakuwa na sanduku lake la kupigia kura,” alisema
Makinda na bila kufafanua, hali iliyowafanya baadhi ya wajumbe kushangaa
uratatibu huo kwani kwa kawaida chaguzi za kumpata mwenyekiti na makamu wake
hufanyika kwa wajumbe kupiga kura kwa ujumla, bila kufuata utaratibu wa mikoa.
Uamuzi huo ulikuja wakati kukiwa na taarifa kwamba baadhi ya
wajumbe, walikuwa wamepanga kumpigia kura za maruhani, mwenyekiti wa chama
hicho, Rais Kikwete.
Dalili kuwa CCM kiligundua njama za hujuma hiyo, zilionekana
mapema wakati Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Yusuf Makamba alipokuwa akimwombea
kura Rais Kikwete.
Makamba na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Vuai Ali Vuai
waliteuliwa na NEC ya CCM kumwombea kura Rais Kikwete kwa wajumbe wa mkutano
huo.
Makamba aliwataka wajumbe wote kumpigia kura za ndiyo Rais
Kikwete kwani wakipiga kura za maruhani wanataka mwenyekiti awe nani.
“Mpigie kura za ndiyo mwenyekiti wetu Kikwete, wale ambao
mnataka kupiga kura za maruhani mnataka mwenyekiti awe nani?” alihoji Makamba,
huku wajumbe wakimshagilia. Viongozi waliotarajiwa kuchaguliwa ni Mwenyekiti wa
CCM na makamu wake wawili kutoka Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.
Waliopendekezwa na Halmashauri Kuu kuwania nafasi hizo ni
Rais Kikwete kwa nafasi ya mwenyekiti, wakati Philip Mangula na Dk Ali Mohamed
Shein walipendekezwa kwa nafasi za umakamu wa Bara na Visiwani sawia. Hadi
tunakwenda mitamboni, matokeo ya uchaguzi huo yalikuwa bado yanasubiriwa.
Hii itakuwa ni mara ya pili kwa CCM, katika uchaguzi huu
kuziba mwanya wa kufanyika hujuma, baada ya Jumapili kubadilisha ghafla ratiba
yake ya uchaguzi na kuanza na uchaguzi wa wajumbe wa Nec, badala ya uchaguzi
huo kufanyika jana.
Hali hiyo iliwafanya wagombea na wapambe wao kushindwa
kupata muda mrefu wa kufanya kampeni ikiwamo kutoa rushwa.
Makamba atikisa
Akitumia aya zilizopo katika vitabu vitakatibu vya Biblia na
Koran, Makamba aliwambia wajumbe wa mkutano huo kuwa Rais Kikwete ana wito wa
Mungu.
“Tembo hashindwi kubeba mikonga yake miwili, sasa wanaosema
kuwa tupige kura za maruhani wanataka awe nani, nasema washindwe kabisa kwa
jina la Yesu,” alisema Makamba huku akishangiliwa kwa nguvu na wajumbe wa
mkutano na baadhi yao waliinuka kwenda kumtuza fedha.
Wakati anatuzwa alikatisha hotuba yake kwa muda, hali ambayo
iliwafanya wajumbe kulipuka kwa kicheko akiwamo Rais Kikwete, huku yeye
mwenyewe akisema, “Ninakula sehemu yangu kama watu wa dini wanavyokula sehemu
yao.”
Mbali na hilo, aliwakumbusha machungu baadhi ya wanaCCM
waliogombea nafasi za ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) kwa kusema wako mbali na
watu na ndiyo baadhi yao waliadhibiwa kwa kunyimwa kura.
Makamba alisema kuwa Rais Kikwete yupo karibu na watu na
kwamba muda wote amekuwa akitekeleza Ilani ya chama hicho, hivyo apewe nafasi
nyingine ya kukiongoza chama hicho.
“Wengine wanapiga kelele kuwa tupunguze kura za mwenyekiti,
lakini wanasahau kuwa wao wana kazi moja, lakini kazi hizo zinawashinda, sasa
kelele ya nini ndugu zangu, mpeni Jakaya mtu wa watu,” alisema.
Alisema CCM imesajili wachezaji wazuri ambao ni watendaji
waliopatikana katika chaguzi mbalimbali za chama hicho na kwamba sasa
wanatafuta kocha wa timu ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho, Rais Kikwete.
Makamba aliwasuta baadhi ya viongozi wa mikoa akisema kama
asingekuwa Rais Kikwete kuwakumbuka hivi sasa hawangepata uongozi, hivyo wanapaswa
kuonyesha shukrani kwa kuisaidia CCM kutekeleza Ilani yake.
Aliongeza kuwa wako watu ambao wamekuwa wakijitafutia
umaarufu mkubwa ikiwamo kutaka uongozi wa nafasi ya urais, lakini hawajipimi
kama wanakubalika au la.
Alisema watu wana namna hiyo wanaweza kufika mahali
wakajikuta wanapigiwa kura na watu wachache sana ikiwamo kura zao na wake zao
kutokana na kuamua kufanya mambo bila ya kufanya tathmni.
Makamba alisema kiongozi ili upendwe na wananchi lazima
ufanye kazi nzuri, kama aliyoifanya Rais Kikwete katika uongozi wake katika
CCM.
Akiwa ameliteka jukwaa la wajumbe huku akishangiliwa kwa
nguvu huku akiendelea kutuzwa, Makamba aliwatolea mfano baadhi ya wenyeviti na
kueleza namna wengine walivyolia wakati wakitafuta nafasi hizo.
“Mfano ndugu yangu Kaborou (Walid, Mwenyekiti wa CCM) kule
Kigoma ulikuwa ukinitukana, lakini leo upo hapa, Shekifu (Henry, Mwenyekiti
Mkoa wa Tanga) kule Tanga ulihangaika sana, Madabida (Ramadhan, Mwenyekiti wa
Mkoa Dar es Salaam) ulikuwa ukihaha kweli, lakini wewe Msukuma Mgeja, (Hamis,
Mwenyekiti wa Mkoa wa Shinyanga) ulilia machozi kabisa, kwa nini leo mwenzenu
anapotafuta nafasi hiyo mnakuwa na nongwa,” alisema.
Hata hivyo, hakufafanua jinsi viongozi hao wanavyohusika
katika mchakato wa uchaguzi huo.
Kabla ya kuingia CCM, Kaborou alikuwa Mbunge wa Chadema wa
Kigoma Mjini, huku Mgeja, Shekifu na Madabida walikabiliwa na upinzani mkubwa
wakati wa uchaguzi wa nafasi zao.
Mstaafu huyo alitumia nafasi hiyo kuwatupia kombora baadhi
ya wasaidizi wa Rais Kikwete kuwa wamelewa madaraka kiasi kwamba hata
wakipigiwa simu huwa hawapokei na badala yake huwapa wake zao simu hizo,
tofauti na Kikwete ambaye kupokea simu wakati wowote.
Hata hivyo, Makamba mbali ya kumnadi Kikwete alitumia jukwaa
hilo kutoa dukuduku lake kuwa kilichomgarimu wakati akiwa ndani ya chama hicho
ni kutokana na kusema ukweli.
Alisema kuwa amekuwa akisimamia katika ukweli na haki wakati
wote jambo ambalo halikukubalika na watu wengi ndani ya chama.

No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA