MGOGORO WA TANZANIA NA MALAWI KUHUSU ZIWA NYASA KUTATULIWA NA MAHAKAMA YA KIMATAIFA.
![]() |
| Waziri wa mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe. |
SERIKALI imesema kuwa itafanya mazungumzo ya mwisho na Malawi
kuhusu mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa, kabla ya kulifikisha suala hilo katika Mahakama ya
Kimataifa ya Haki (ICJ) ili kupatiwa ufumbuzi baada ya pande hizo mbili
kushindwa kukubaliana.
Imesisitiza kuwa Nyasa ni urithi wa nchi tatu, yaani Tanzania, Malawi na Msumbiji na hivyo siyo
sahihi upande wowote kati ya nchi hizo kudai unamiliki sehemu kubwa ya ziwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mara baada ya
kukutana na mabalozi wa nchi za Umoja wa Ulaya nchini (EU) katika Ukumbi wa
Karimjee Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe alisema kuwa tayari ujumbe kutoka Malawi umeshafika nchini kwa
ajili ya mazungumzo hayo ambayo yamepangwa kufanyika kesho.
Waziri Membe alikutana na mabalozi kutoka nchi za Umoja wa
Ulaya kuwapa taarifa juu ya mambo yanayoendelea nchini zikiwamo vurugu za
kidini zilizojitokeza hivi karibuni.
Katika mazungumzo hayo, Waziri Membe pia aliwaeleza
wanadiplomasia hao kuhusiana na hali ya uhuru wa vyombo vya habari nchini,
uamuzi wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) kujihusisha
mzozo unaoendelea huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), pamoja na mzozo
wa mpaka wa Ziwa Nyasa.
“Lakini pia nilikutana na mabalozi hao kuwaelezea hali ngumu
ya uchumi wa nchi za ulaya na jinsi inavyoathiri maendeleo ya nchi za Afrika, “
alisema Waziri Membe na kuongeza kuwa:
“Timu ya Malawi
ipo nchini kwa mazungumzo na keshokutwa (kesho) kutakuwa na mkutano wa mawaziri
wa Mambo ya Nje wa nchi hizi mbili kuzungumzia chanzo cha mgogoro huu wa Ziwa
Nyasa. Katika mkutano huo tutazungumzia tunakoelekea kwa kuwa tofauti zetu zipo
wazi,” alisema Membe.
Alisema watakaoalikwa katika mkutano huo ni Mwanasheria Mkuu
wa Serikali (AG) Frederick Werema na Waziri wa
Sheria, Mathias Chikawe na kwamba lengo la kuwaalika viongozi hao ni kutaka
kulikabidhi suala hilo
katika vyombo vya sheria.
“Baada ya mazungumzo tutasubiri baraka za Rais Jakaya
Kikwete ambaye pia atashauriana na Rais wa Malawi, Joyce Banda ili kukubaliana
suala hili liende ICJ,” alisema Membe.
Alisema kuwa kabla ya
kuchukua hatua hizo ni lazima wakutane na ujumbe huo kutoka Malawi.
“Timu ya Tanzania
ambayo ipo makini inajipanga kwenda Umoja wa Ulaya, Uingereza na Ujerumani kwa ajili ya kupata
nyaraka zote za ushahidi na baada ya hapo utaanza mchakato wa kwenda ICJ,”
alisisitiza.
Alisema kuwa mabalozi hao wamefurahia jinsi Tanzania inavyotatua mgogoro huo na Malawi
kwa kutumia njia za kidiplomasia zaidi.
Fidelis Butahe
Source: MWANANCHI

No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA