CHADEMA YASAMBAZA PIKIPIKI NCHI NZIMA.
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza
mkakati wa Uchaguzi Mkuu 2015 kikiahidi kumwaga pikipiki katika tarafa zote
nchini kwa ajili ya kuwafikia wananchi kuelekea uchaguzi huo.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema hayo jana
katika kikao cha viongozi wa chama hicho na wadau wake kilichofanyika hapa.
Mbowe alisema pikipiki hizo zitakuwa na vipaza sauti maalumu
zitawasaidia viongozi wa chama hicho kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
“Tumeanza mkakati wa kuhakikisha tunawafikia wananchi kila
mahali. Tunataka kusikiliza matatizo yao,
na hata pale ambako kuna shida ya usafiri, kwa pikipiki tutafika,” alisema.
Tayari chama hicho kimezindua kampeni yake ya Vuguvugu la
Mabadiliko (M4C), ambayo lengo lake
ni kuwaandaa wananchi kwa
uchaguzi ujao.
Mbowe alisema upatikanaji wa pikipiki hizo unatokana na
fedha za ruzuku ambazo zinatolewa na Serikali kwa chama hicho pia marafiki na wanachama wake walioko nje ya
nchi.
Aliwataka viongozi wa chama hicho katika ngazi zote kufanya
kazi kwa kujituma ili kuhakikisha kinashika dola mwaka 2015.
“Tanzania
inahitaji mabadiliko na sisi tukiwa viongozi tunapaswa kujipanga kwanza,
kuhakikisha tunaongeza wanachama pia kuzitatua kero za wananchi,” alisema
Mbowe.
Katika mkutano huo, Mbowe aliwapongeza viongozi wa Chadema,
Wilaya ya Hanang’ kwa kazi kubwa waliyoifanya kiasi cha kupata na madiwani 17
katika halmashauri hiyo.
Awali, Mbunge wa Viti Maalumu, Mkoa wa Manyara, Rose Kamili
alisema chama hicho kimejipanga kutwaa Jimbo la Hanang’ katika uchaguzi ujao na
Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’.
“Katika miaka hii mitano Chadema, Hanang’ tumekuwa na
mafanikio makubwa na hili linatokana na mshikamano mkubwa wa viongozi katika
ngazi mbalimbali,” alisema.
Chanzo: MWANANCHI.

No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA