WALIMU TANZANIA WAGOMEA SIKU YAO: (Kitaeleweka tu Mkitulazimisha)
Asili Yetu © All rights reserved
![]() |
| Mgomo wa waalimu. |
CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) kimegoma kushiriki
maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani inayoadhimishwa leo kwa madai kina huzuni
na hakina mafanikio yoyote ya kuwaambia walimu.
Aidha, chama hicho kimetoa mwito kwa Serikali kukubali
ushauri wa Bunge na uamuzi wa Mahakama, ili warudi katika meza ya majadiliano
kwa ajili ya kuendeleza walipoachia.
Katibu wa CWT, Ezekiel Oluoch alisema hayo jana Dar es
Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho hayo ambayo
kaulimbiu yake ni ‘Kuwatetea walimu’.
“Kesho (leo) ni Siku ya Walimu Duniani, kwa bahati mbaya
hatutakuwa na sherehe ama maadhimisho kwani hakuna chochote cha kuelezea …
hatuwezi kusherehekea tukiwa na matatizo mengi ambayo hayajafikia suluhu,”
alisema Oluoch na kuongeza kuwa wataadhimisha siku yao wakiwa kazini na
wamekata tamaa.
Alisema mwajiri wao ambaye ni Serikali hajalipa madai ya
wakufunzi wa vyuo vya ualimu, hajashughulikia madai ya walimu ambayo hayajalipwa
na kutoajiri walimu waliohitimu ingawa fedha zimetengwa na Bunge.
Alisema katika siku hiyo, CWT inatoa mwito kwa Watanzania na
jumuiya za kimataifa kujitokeza kutetea walimu dhidi ya manyanyaso wanayopata
kutokana na mishahara duni isiyokidhi mahitaji muhimu ya kila siku.
Pia alitaka walimu kushikamana katika kudai maslahi bora
zaidi kama watumishi wengine wa umma na Serikali ilipe madeni yote wanayodai
walimu, wakufunzi wa vyuo vya ualimu nchini pamoja na wakaguzi wa shule.
Kuhusu kurudi katika meza ya majadiliano, Rais wa CWT,
Gratian Mukoba alidai Serikali imegoma kukutana na chama hicho kama
ilivyoagizwa na Mahakama na Bunge.
Alisema pamoja na leo kuwa Siku ya Walimu, Serikali imekataa
mapendekezo ya CWT ya kuteua timu ya majadiliano nje ya chombo cha majadiliano
ya pamoja kwenye utumishi wa ualimu ili madai ya walimu yashughulikiwe ndani ya
mwaka huu wa fedha.
“Hadi sasa Serikali imekiuka amri ya Mahakama ya Kazi ambayo
iliagiza pande zote, yaani CWT na Serikali zirudi kwenye meza ya majadiliano…
kwa uelewa wetu, meza iliyokuwa inatumika kwa majadiliano kabla ya mgomo ndiyo
inayostahili kutumika kuendeleza mazungumzo kati ya pande hizi,” alisema
Mukoba.
Alisema CWT inalaani kwa nguvu zote ukaidi huo wa Serikali
ambao hauna tija kwa nchi, bali unazidi kuwasababishia walimu kuishi maisha
magumu yasiyo na mfano na kudhulumu wanafunzi haki yao ya kupata elimu.
Akijibu hoja ya Serikali kukaidi uamuzi wa Mahakama na
Bunge, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina
Kombani alisema Serikali inapanga tarehe mwafaka ya kukutana na kwamba
haijakaidi agizo hilo.
Alisema baada ya CWT kuwaandikia wako katika majadiliano na
kwamba wameahidi kukutana ili kuzungumza.
CHANZO: HABARILEO

No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA