VURUGU KUBWA ZILIZOTOKEA ZANZIBAR NA DAR: MAGARI, BAA VYACHOMWA MOTO, NI BAADA YA KIONGOZI WA UAMUSHO KUTEKWA, PIA SHEHE PONDA KUTIWA MBARONI
Asili Yetu Tanzania.Copyright
POLISI mkoani Dar
es Salaam na wale wa Kisiwani Zanzibar, jana walitumia
mabomu ya machozi na maji ya kuwasha kusambaratisha makundi ya watu wanaodaiwa
kuwa waumini wa Dini ya Kiislamu, waliopanga maandamano kushinikiza kuachiwa
kwa viongozi wao.
Kisiwani Zanzibar vurugu kubwa ziliibuka baada ya kusambaa
taarifa kuwa Kiongozi wa Kundi la Uamsho, Sheikh Farid Hadi Ahmed alitekwa
nyara juzi saa 3 usiku akiwa kwenye gari lake na
dereva wake.
Vurugu hizo zilisababisha uharibifu wa mali kadhaa
ikiwamo Maskani Kaka ya Kisonge inayomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM)
ambayo ilichomwa moto na waandamanaji.
Waandamanaji hao pia walichoma moto baa za Darajani na
Mbawala eneo la Mikunguni na baadhi ya nyumba za kulala wageni, kabla Vikosi
vya Kutuliza Ghasia (FFU) na Kikosi cha Zima Moto kudhibiti vurugu hizo kwa
mabomu ya kutoa machozi.
Pia magari kadhaa yalichomwa moto na kuharibiwa vibaya
yakiwa yameegeshwa katika maeneo mbalimbali, huku mipira na matairi vikichomwa
katika barabara kadhaa.
Katika maeneo ya Mjini baadhi ya njia zilifungwa na watu
waliokuwa wakitoka kazini walishindwa kwenda nyumbani. Maeneo yaliyoathirika
zaidi ni yale ya Malindi, Darajani hadi Michenzani ambako njia zilifungwa na
mabomu yalisikika yakipigwa mfululizo.
Katibu wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu
Zanzibar (Jumiki), Sheik Abdallah Said alisema,
“Taarifa tulizonazo ni kwamba Sheikh Farid ametoweka katika
mazingira ya kutatanisha…Alitoka kwake Mbuyuni katika gari yeye na kijana wake
wa hapo nyumbani, lakini baadaye kuna gari ikamfuata na kusimama na ndipo
alipoingia katika hilo
gari jingine na hakuonekana tena. Hatujui ni kina nani waliomchukua na hatujui
ilikuwaje akaingia katika hilo
gari ...”
Polisi waliimarisha ulinzi katika baadhi ya maeneo hasa
Msikiti wa Mbuyuni ambao uko jirani na makazi ya Sheikh Farid. Kamishna wa
Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema polisi halihusiki na kukamatwa kwa
Farid, lakini wao wanaamini kwamba ‘amejipoteza’ mwenyewe na kujificha.
Kamishna Mussa alisema polisi watawasaka wote waliosababisha
vurugu hizo, na kwamba hadi sasa hawafahamu chanzo chake bado.
“Tunafanya uchunguzi zaidi kujua chanzo cha fujo hizo ingawa
mimi sijui habari za kutekwa Farid, sasa tunasema tunachunguza chanzo cha
vurugu hizo na tukishapata uthibitisho na waliosababisha tutawafikisha
mahakamani kujibu mashtaka,” alisema kamishna huyo.
Ilivyokuwa Zanzibar
Vurugu hizo zilianza katika maeneo mbalimbali muda mfupi
baada ya vijana kadhaa kukusanyika katika eneo la Darajani kando ya Soko Kuu
majira ya asubuhi, kutokana na kuzagaa kwa taarifa kwamba Sheikh Farid alikuwa
haonekani.
Idadi ya vijana hao ilikuwa ikiongezeka kadiri muda
ulivyosonga, huku wengi wao wakiwa na silaha za aina mbalimbali zikiwamo
magongo na mawe, hali iliyoibua hofu kwa wafanyabiashara wa eneo hilo, hivyo baadhi yao
waliamua kufunga maduka.
Maeneo yalioharibiwa ni pamoja na baadhi ya nyumba za kulala
wageni ambazo zimechomwa moto katika eneo la Amani, huku baadhi ya vijana
wakionekana wakikimbia na kreti za pombe.
Katika eneo la Darajani, vijana kadhaa wakishirikiana na
Wamachinga, walionekana wakivunja kisha kuingia katika moja ya maghala ya
kuhifadhia bia, ambako walipora bidhaa zote zikiwamo kreti kadhaa za bia
zilizokuwa zimehifadhiwa humo.
Baadhi ya wenye maduka walifunga na kutoweka, lakini
waporaji waliiba baadhi ya bidhaa vikiwamo vyakula, kisha kutokomea navyo kusikojulikana.
Katika maeneo ya Ng’ambo ambayo ni Amani, Mikunguni,
Kwerekwe na Daraja Bovu vijana walioonekana kuwa na hamasa, waliingia kwenye makazi
ya watu na kuiba vitu kadhaa, na kila mabomu yalipopigwa walikimbilia
vichochoroni na baada ya muda walirejea tena.
Maeneo ya Malindi, Michenzani na Rahaleo, kulikuwa na vurugu za urushaji mawe
na kusababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu katika maeneo hayo.
Matawi ya miti ilikatwa na kuunganishwa na magari mabovu
kuwekwa barabarani kisha kuchomwa moto. Hali hiyo ilisabababisha uharibifu
mkubwa katika baadhi ya barabara, na katika fujo hizo baadhi ya vijana
walikamatwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Azizi Juma
Mohammed alithibitisha kutokea kwa fujo hizo na kusema Jeshi la Polisi
linafanya uchunguzi kujua chanzo chake na taarifa kamili zitatolewa baada ya
kukamilika uchunguzi huo.
Ponda Dar
Jijini Dar es
Salaam, baadhi ya watu walipanga kufanya maandamano
hadi Makao Makuu ya Polisi, kupinga kukamatwa kwa Katibu wa Jumuiya na Taasisi
za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda aliyekamatwa juzi usiku na kushikiliwa
kutwa nzima ya jana katika Kituo Kikuu cha Polisi.
Ponda alitiwa mbaroni kwa tuhuma za kuchochea vurugu na
uvunjifu wa amani jijini Dar es Salaam,
na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisisitiza
kuwa polisi wamechoka kuvumilia harakati zake za kutaka “nchi isitawalike”.
“Kuanzia leo uvumilivu kwa Jeshi la Polisi dhidi ya watu
wasiofuata sheria za nchi umekwisha. Kwa kuwa Ponda ni mtu anayepotosha watu
waliopo chini yake wanaotaka kuandamana bila utaratibu wasitulaumu kwa lolote
lile litakalotokea,” alisema Kova.
Kova alisema hadi jana Ponda alikuwa bado anahojiwa katika
Kituo Kikuu cha Polisi, Mkoa wa Dar es
Salaam na kwamba ushahidi ukijitosheleza, atafikishwa
mahakamani wakati wowote.
Alisema taasisi anayoingoza Sheikh Ponda haijasajiliwa kwa
mujibu wa sheria kufanya shughuli za dini. Hivyo basi shughuli zote
zinazoendesha na taasisi hiyo si halali.
"Natoa wito pia kwa wafuasi wa kiongozi huyo,
walioshiriki katika vurugu mbalimbali za hivi karibuni, wajisalimishe haraka
kwa kuwa sasa tupo katika mchakato wa kuwasaka, kuwakamata na baadaye kuwafikisha
mbele ya sheria," alisema.
Tuhuma za Ponda
Kamanda Kova alidai kuwa Sheikh Ponda amekuwa akichochea
vurugu na kuwashawishi wafuasi wake kuidharau Serikali na vyombo vya usalama.
“Ponda amekuwa ni mtu ambaye amefanya nchi hii, hasa katika
Jiji la Dar es Salaam
kukaa katika hali ya wasiwasi. Ijumaa imekuwa siku ya fujo badala ya kuwa siku
ya amani,” alisema Kova.
Alisema vurugu hizo zinazoongozwa na Sheikh Ponda zimekuwa
zikisababisha baadhi ya watu kushindwa kwenda kazini siku za Ijumaa na hali
hiyo haivumiliki tena.
Kamanda Kova alitaja tuhuma nyingine dhidi ya Sheikh Ponda
kuwa ni kuongoza kundi la watu kwenda kuvamia kiwanja namba 311/3/4 eneo la
Chang’ombe ambacho kinamilikiwa na
kampuni Agritanza.
"Kiwanja alichokwenda kukivamia kilikuwa mali ya Baraza
Kuu la Waislamu nchini (Bakwata) na kiliuzwa kihalali kwa kampuni hiyo,"
alisena.
Alitaja tuhuma nyingine kuwa ni kufanya maandamano kinyume
cha sheria, ikiwamo kuweka kambi Makao Makuu ya Polisi bila kibali cha jeshi hilo wiki kadhaa
zilizopita.
Kamanda huyo alisema Ponda anashikiliwa pia kwa kuwa mstari
wa mbele kupambana na vyombo vya dola na
Serikali, ikiwa ni pamoja na kushawishi wafuasi wake kumdharau Rais wa nchi.
“Vilevile amekuwa akiendesha maandamano na kukusanyika
Kiwanja cha Kidongo Chekundu, huku wakijitapa kuwa wana nguvu zaidi ya Jeshi la
Polisi,” alieleza Kova.
Polisi pia wanamtuhumu Ponda kwa kuanzisha vurugu na vitisho
dhidi ya Sheikh Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Mufti Shaaban
Bin Simba na kutaka kumtoa madarakani kwa nguvu pamoja na kutaka kuvamia ofisi
yake.
Alikamatwaje?
Kamanda Kova alisema Ponda alikamatwa na askari waliomuwekea
mtego kutokana na yeye kuwa bingwa wa kutoroka kila akifanya matukio.
“Askari waliowekwa maalumu kwa ajili ya kumkamata
walifanikiwa kumtia nguvuni saa 4:00 usiku karibu na eneo la maficho yake
ambako alipelekwa na pikipiki,” alisema Kova.
“Hivi Ponda ni nani mpaka awe na uwezo wa kumpa Rais
aliyechaguliwa na wananchi siku saba kuwaachia watu waliopo mahakamani yeye
amechaguliwa na nani kuongoza taasisi aliyonayo na anatoa wapi nguvu za kufanya
mambo yote hayo?,” alihoji Kova.
Alisema kulingana na matukio anayoyaongoza Ponda, wananchi
wameanza kuona kama anaogopwa na vyombo vya
dola, jambo ambalo siyo kweli.
Aliongeza kuwa polisi wana uwezo wa kumdhibiti, isipokuwa
walikuwa wanatumia busara tangu alipoanza vurugu na kwa sasa uvumilivu
umewashinda, hivyo wataanza kumshughulikia.
Vurugu zazuka
Kukamatwa kwa Sheikh Ponda kulizua vurugu jijini Dar es
Salaam na kufanya baadhi ya wakazi wake hasa maeneo ya Mnazi Mmoja na Kariakoo,
kuingiwa kiwewe baada ya polisi kutumia mabomu ya machozi na maji ya kuwasha
ili kuwasambaratisha watu waliokuwa wanataka kuandamana kwa lengo la
kushinikiza kiongozi huyo aachiwe.
Hali hiyo ilisababisha watu kukimbia ovyo katikati ya iji na
kuongezeka kwa misongamano ya magari, jambo lililofanya usafiri wa daladala
kuwa mgumu kwenda na kutoka katikati ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam.
Baadhi ya wafanyabiashara walifunga maduka yao
wakihofia kuporwa mali
wakati wa vurugu hizo, baada ya vibaka kujichanganya wakijaribu kufanya uhalifu
huo.
Katika eneo la Mnazi Mmoja, polisi walirusha maji ya kuwasha
kusambaratisha kundi la watu hao, huku wengine wakiwa wanadhibitiwa walipokuwa
wakienda Makao Makuu ya Polisi ili kumtoa kiongozi huyo.
Baadhi ya mashuhuda walisema, mbali na Ponda watu hao
walikuwa wanataka kwenda polisi kuwatoa watu waliokuwa wanashikiliwa kituoni
hapo kwa tuhuma za kufanya vurugu na kuharibu makanisa katika Kata ya Mbagala
wilayani Temeke.
Chanzo:Mwananchi.

No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA