MAASKOFU KKKT WATOA TAMKO ZITO DHIDI YA UCHOMAJI WA MAKANISA DAR.
Asili Yetu Tanzania.Copyright
MAASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT), wamelaani uharibifu uliofanyika
katika makanisa ya Mbagala, Dar es Salaam na kukemea vitendo hivyo viovu.Kauli
ya maaskofu hao ilitolewa katika tamko lao lililosainiwa na maaskofu 20 wa
kanisa hilo, wakiongozwa na Mkuu wa KKKT ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya
Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa.
Kabla ya kutoa tamko hilo,
Dk Malasusa aliwaongoza maaskofu hao kutembelea kanisa la KKKT Usharika wa
Mbagala ambalo lilichomwa moto na watu wanaodhaniwa kuwa waumini wa dini ya
Kiislamu, Oktoba 12 mwaka huu.
Walisema wamelazimika kuonya
uvunjifu huo wa amani uliofanywa kwa mgongo wa uanaharakati
wakitahadharisha kuwa, uvumilivu wao usitumike kuvunja sheria za nchi. “Tanzania yenye
amani na mshikamano ni tunda la dini zote, makabila yote, itikadi zote za
vyama, rangi zote na hali zote za kiuchumi. Hata wasio na dini wanachangia
amani ya nchi hii,” linasema tamko hilo.
Maaskofu hao walisema kwa macho na masikio yao, wameendelea
kushuhudia vitendo vya uchomaji makanisa huko Zanzibar, Mwanza, Mdaula, Mto wa
Mbu, Tunduru, Rufiji, Kigoma na sasa Mbagala. Walisema wakati wote uvumilivu wa
Wakristo huenda umetafsiriwa kuwa ni unyonge na woga. “Sisi maaskofu wa KKKT,
tumepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za matukio ya uchomaji wa makanisa katika
eneo hili la Mbagala.
”Tumekuwa katika mkutano wetu wa Mwaka wa Lutheran Mission
Cooperation (LMC) huko Moshi pamoja na vyama vyote vya Kimisionari vya Ulaya na
Marekani. Tumelazimika kukatisha mkutano huo kujionea yaliyotokea Mbagala,”
lilieleza tamko hilo.
Katika tamko hilo maaskofu hao walieleza kuwa
dalili za mateso ya kimbari kama ilivyo kwa
mateso ya kanisa; zilianza kitambo na hazikushughulikiwa na waliomrithi Baba wa
Taifa.“Dalili hizo ni kama madai yasiyo ya kawaida na ya mara kwa mara kwa
Serikali inayodaiwa kutokuwa na dini ambayo ni kama, kulazimisha uvaaji wa
alama za kidini katika taasisi za umma ili kurahisisha na kuratibisha tofauti
za Watanzania,” wameeleza na kuongeza:
“Tunajiuliza likitokea la Mbagala katika shule zetu na vyuo
vya umma, watachomwa wangapi na kuuawa wangapi?”Wameendelea kueleza madai na
mashinikizo ya uanzishwaji wa mahakama za kidini hapa nchini, mashinikizo ya
kidini yanayoingilia mifumo ya kitaaluma na kisheria na mashinikizo ya kidini
juu ya mfumo wa uteuzi wa watendaji wa Serikali na katika ofisi za umma ni
madai yenye matatizo.
“Tumeshuhudia wizara zetu zikivamiwa mchana kweupe na
kushinikiza kuachiwa kwa watuhumiwa wa uhalifu; tumeshuhudia vituo vya polisi
vikichomwa moto; mahakama zikilazimishwa kufunga shughuli zake, misikiti
ikitekwa, uhai wa viongozi wa dini ukitishiwa hadharani na viongozi wastaafu
wakizabwa vibao hadharani kwa sababu zinazoitwa harakati za kidini. Tumefikia
kuhoji, watu hawa wavamie nini ndipo hatua zichukuliwe?”Wamehoji wanataka kichomwe nini ndipo viongozi wenye
dhamana ya kulinda mali na uhai washtuke au auawe nani ndipo iaminike kuwa watu
hawa ni tishio kwa usalama wa taifa letu.Wamesema wanawasihi waumini wa dini na Watanzania kwa jumla,
wenye wajibu wa kutii na wasiolazimika kutii, kuzingatia kuwa Mwenyezi Mungu
analipenda taifa hili na watu wake.
Kamwe hawezi kuliacha liangamie.Mbali na Dk Malasusa
maaskofu wengine waliotia saini tamko hilo ni pamoja na Askofu wa Dayosisi ya
Kaskazini Mashariki, Dk Stephen Munga, Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, Dk
Martin Shao, Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk Thomas Laizer na
Askofu wa Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza.Wengine ni Askofu wa Dayosisi ya Kusini, Isaya Mengele,
Askofu wa Dayosisi ya Kusini Kati, Levis Sanga, Askofu wa Dayosisi ya
Kaskazini Magharibi, Elisa Buberwa, Askofu wa Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa
Victoria, Andrew Gulle na Askofu wa
Dayosisi ya Mkoani Mara, Michael Adam. Wengine ni Askofu wa Dayosisi ya
Ulanga-Kilombero, Renard Mtenji , Askofu wa Dayosisi ya Konde, Dk Israel-Peter
Mwakyolile, Askofu wa Dayosisi ya Kusini Magharibi, Job Mbwilo, Askofu wa
Dayosisi ya Iringa, Dk Owdenburg Mdegella na
Askofu wa Dayosisi ya Morogoro, Jacob Ole Mameo.Katika tamko hilo pia
wako Askofu wa Dayosisi ya Mbulu, Zebedayo Daudi, Askofu wa Dayosisi ya Meru,
Paulo Akyoo, Askofu wa Dayosisi ya Pare, Charles Mjema, Askofu Mteule wa Dayosisi ya Dodoma, Amon
Kinyunyu na Askofu Mteule wa Dayosisi ya Kati, Dk Alex Mkumbo.
Kanisa jingine lachomwa
Wakati maaskofu hao wakitoa tamko hilo, kanisa jingine limechomwa moto jana baada ya kijana mmoja
asiyefahamika kutumbukiza kaa la moto
ndani ya kanisa la Furaha International Gospel Church lililoko Yombo
Makangarawe na kusababisha kuteketea kwa
baadhi ya vifaa vya muziki.
Akizungumza na Mwananchi baada ya tukio hilo, Kamanda wa Mkoa
wa Temeke, David Misime alisema tukio hilo limetokea kanisa likiwa limefungwa
na wachungaji hawakuwapo kanisani hapo.
“Kanisa lina madirisha ya vitundu kwa hiyo yule kijana
alipitisha mkono akaweka moto huo kwenye meza iliyokuwa na vifaa vya muziki,
huu ni uchunguzi wa awali na chanzo kinadhaniwa kuwa ni hicho,”alisema na
kuongeza kuwa juhudi za majirani
zilisaidia baada ya kuvunja mlango wa kanisa hilo na kuingia ndani ambapo
walifanikiwa kuuzima moto huo na kwamba, hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa.
“Kwa hiyo tusihukumu moja kwa moja kwamba kanisa limechomwa
moto na watu fulani kwa sababu hatujathibitisha, tunafanya uchunguzi ili
kubaini ukweli,” alisema Masime.
Boniface Meenana Kelvin Matandiko
No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA