DAWA BANDIA ZA KUPUNGUZA MAKALI YA UKIMWI - MKURUGENZI WA MSD ASIMAMISHWA KAZI.
Asili Yetu Tanzania.Copyright
Makopo ya dawa za kupunguza makali ya Ukimwi yakitofautiana
vifungashio. Kopo la kwanza kushoto linaonyesha dawa halisi ya kupunguza makali
ya Ukimwi iliyokidhi viwango ikifuatiwa na makopo 3 yenye dawa bandia ya
kupunguza makali ya Ukimwi yenye jina la biashara TT –VR 30 toleo namba
0c.01.85 yaliyotengenezwa na kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries
Ltd. (Picha na Aron Msigwa – MAELEZO).
Serikali imewasimamisha kazi mkurugenzi mkuu wa Bohari ya
Dawa nchini (MSD) ,Mkuu wa kitengo cha Udhibiti na Ubora na Afisa Udhibiti
Ubora wa ohari hiyo ili kupisha uchunguzi dhidi yao kufuatia kuruhusu
kusambazwa kwa dawa bandia za kupunguza makali ya UKIMWI aina ya TT –VIR 30
katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya nchini.
Aidha imepiga marufuku usambazaji na matumizi ya dawa aina
ya TT –VIR 30 toleo na 0C .01.85 inayotengenezwa na kiwanda cha Tanzania
Pharmaceutical Industries Ltd (TPI) kufuatia dawa hiyo kutengenezwa chini ya
kiwango na kutofaa kwa matumizi ya binadamu.
Akizungumza leo jijini Dar es salaam Waziri wa Afya na
Ustawi wa Jamii Dkt. Hussein Mwinyi amesema kuwa hatua hiyo imechukuliwa mara
baada ya kubaini kuwepo kwa dawa bandia ya kupunguza makali ya Ukimwi katika
hospitali ya wilaya ya Tarime kufuatia ukaguzi uliofanywa na Wizara ya Afya
kupitia Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA).
Amesema kuwa ukaguzi na uchunguzi wa kimaabara dhidi ya dawa
hiyo isiyokidhi viwango ulibainia kuwa nyaraka zilizopo kuhusiana na dawa hizo
unaonyesha kuwa Kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd (TPI)
waliiuzia Bohari ya Dawa (MSD) dawa hiyo bandia toleo namba 0C. 01. 85
iliyotengenezwa nchini mwezi Machi 2011 na kuonyesha mwisho wa matumizi yake
mwezi Februari 2013.
Amefafanua kuwa dawa hiyo bandia ilikua na dawa zenye rangi
mbili tofauti njano na nyeupe na kuwa na viambata tofauti vilivyopaswa kuwepo
aina ya Efaverenz badala ya Niverapine, Lamivudine na Stavudine na kuongeza
kuwa vidonge vilivyokutwa kwenye vifungashio vya dawa husika vilikua tofauti na
vifungashio vilivyosajiliwa na TFDA.
Dkt. Mwinyi amesema kuwa serikali inahakikisha kuwa dawa
zenye ubora unaotakiwa za kupunguza makali ya UKIMWI zinaendelea kupatikana
katika vituo vya kutolea huduma kote nchini na kuwaagiza waganga wakuu wa
mikoa, wilaya na kamati za dawa na Tiba katika vituo vya huduma za afya
kuhakikisha kuwa zinapokea, kuhakiki na kusimamia kikamilifu ubora na matumizi
sahihi ya dawa na vifaa tiba nchini.
Kuhusu upatikanaji wa dawa hizo amewatoa hofu wananchi na
kuwahakikishia kuwa dawa za kutosha zenye viwango stahili zitaendelea
kupatikana katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini na kuwataka wananchi
kutoa kushirikiana na mamlaka husika kwa kutoa taarifa pale wanapobaini kuwepo
kwa dawa zenye ubora wenye mashaka au uvunjifu wa sheria inayosimamia ubora na
usalama wa dawa.


No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA