Asili Yetu © All rights reserved
Wachimba migodi wa kampuni ya Lonmin nchini Afrika Kusini,
wamekubali kurejea kazini siku ya Alhamisi.
Wachimba migodi hao walijawa na furaha huku wakishangilia
walipoambiwa kuhusu pendekezo la asilimia 22 la nyongeza ya mishahara
watakayolipwa.
Lakini shirika la kushughulikia mizozo ya ajira liliambia
BBC kuwa lilikuwa linasubiri ikiwa pendekezo la hivi karibuni la mishahara
litakubalika au la.
Mwezi jana polisi waliwaua kwa kuwapiga risasi wafanyakazi
wa mgodi huo waliokuwa wakigoma kudai mishahara bora na mazingira mazuri ya
kazi. Wachimba migodi 34 waliuawa.
Uzalishaji wa madini umeathirika sana kwa wiki kadhaa huku
mzozo huo ukisambaa hadi katika migodi mingine.
Tume ya maridhiano iliambia BBC kwamba waakilishi wa
wafanyakazi hao, waliwashauri wachimba migodi kuhusu pendekezo la sasa la
nyongeza ya mishahara na wala hawakupata pingamizi zozote.
Wafanyakazi hao , walikusanyika katika uwanja mmoja karibu
na mgodi wa Marikana kusikiliza hotuba ya waakilishi wao.
Wamekuwa wakidai nyongeza ya mishahara ya dola miatisa
thelathini na tano. Kwa sasa wanalipwa kati ya randi 4,000 na 5,000.
''Kilichofanyika leo ni ushindi mkubwa kwa wafanyakazi hawa
na watarejea kazini siku ya Alhamisi'' alinukuliwa akisema kasisi mmoja
aliyewawakilisha wafanyakazi hao, Joe Seoka.
Pia alielezea kuwa wafanykazi hao watalipwa randi 2,000 kwa
kipindi ambacho walikuwa wanagoma kwani hawakuwa wanapokea malipo yoyote.

No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA