WANAFUNZI WA DARASA LA SABA WALIOFANYA VIZURI KATIKA MITIHANI YA KUHITIMU MWAKA 2012.
Florence
Majani
WANAFUNZI walioongoza mtihani wa Darasa la Saba
kitaifa mwaka jana, ni wasichana watatu waliokuwa wanasoma katika Shule ya
Msingi Tusiime iliyoko Dar es Salaam, imefahamika.
Wasichana hao, Justina Kalala, Janeth Kijazi na Kellen
Mudogo waliongoza mtihani huo wenye masomo matano kwa kila mmoja kupata alama
234 kati ya 250.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, mabinti hao ambao
wote wanasoma kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya
Marian, Bagamoyo, walisema siri ya mafanikio yao ni maombi na nia ya kutaka kufaulu.
Justina alisema siri ya kufaulu mitihani yake ni
kumtanguliza Mungu kabla hajafanya kitu chochote hata kama
ni majaribio ya kawaida darasani... “Pia elimu bora ninayopewa na wazazi wangu
nayo inanipa nguvu ya kusoma kwa bidii.”
Justina alisema siri nyingine ya kufaulu kwake katika
mitihani hiyo ni kusoma na kisha kuwafundisha wenzake kile alichokielewa.
Alisema jambo hilo
lilimjengea uwezo wa kuyashika yale aliyoyasoma.
“Nilikuwa nawakusanya wenzangu katika makundi ili tusome.”
Mwanafunzi huyo ambaye alipokuwa shule ya msingi aliteuliwa
kuwa mratibu wa taaluma kutokana na kuwaongoza wenzake katika vikundi vya
kujisomea, alisema anatamani kuwa mfamasia pindi atakapofanikiwa kumaliza
masomo yake na kufaulu.
Pia, Janeth ambaye alisema ufaulu wake ulimtegemea zaidi
Mungu, anapenda zaidi masomo ya sayansi... “Nataka kuwa daktari ndiyo maana
najitahidi zaidi katika masomo ya sayansi. Nilipokuwa shule ya msingi nilikuwa
naweka juhudi zaidi katika somo la hesabu na baiolojia.”
Alisema alipokuwa msingi, alikuwa ni kiongozi wa kikundi cha
kujisomea na alikuwa anatumia muda wake mwingi kusoma vitabu na kuwauliza
walimu kile ambacho alikuwa hakijui.
Kwa upande wake, Kellen mbali na kusema kwamba anamtegemea
Mungu zaidi katika masomo yake, alitoa siri nyingine ya kushinda katika mtihani
huo kuwa ni kurudia kile walichofundishwa na kutumia vyema muda wake.
Kellen alisema anapenda masomo ya sayansi na anatamani kuwa
daktari endapo atafaulu masomo yake ya Chuo Kikuu.
Walikuwa na msukumo
Aliyekuwa mwalimu wa darasa wa wanafunzi hao huko Tusiime,
Valentine John alisema wanafunzi hao walikuwa na msukumo wa ndani wa kusoma
tofauti na wengine.
“Pia wameandaliwa vyema tangu chekechea ndiyo maana
wamefanya vizuri, sisi haitushangazi wao kuongoza kwa sababu tuliujua ubora wao
tangu zamani,” alisema.
Mwalimu huyo alisema wanafunzi hao watatu walikuwa si
wakorofi, bali wasumbufu kwa walimu katika mambo wasiyoyajua.
“Justina anapenda kusoma na kuwaongoza wenzake katika
vikundi vya masomo, Janeth ni mpole lakini anapenda vitabu na Kellen ni mpole,
lakini mwepesi kuuliza pale asipoelewa,” alisema.
Mwalimu Mkuu wa Tusiime, Thomas Samson alisema matokeo hayo
ni mchakato wa ushirikiano kati ya walimu, wazazi na wanafunzi.
Alisema shule hiyo inatumia mfumo wa kumtafiti mtoto
mmojammoja ili kujua namna ya kumfundisha na kubaini kama
ana matatizo ya kifamilia.
“Watoto wanatengwa katika mikondo kutokana na uwezo wao,
wenye alama za juu wanawekwa katika darasa lao ili kuwapa changamoto wengine
waongeze juhudi na pia kuwafundisha kulingana na uwezo wao,” alisema na
kuongeza kuwa kwa sababu hiyo, haishangazi kuona wanafunzi hao wametoka darasa
moja na ni marafiki. Mwalimu wa Taaluma wa Sekondari ya Marian, Flora Mapunda
alisema wanafunzi hao wapo katika hatua nyingine ambayo inahitaji bidii zaidi,
hivyo wanatarajiwa kuonyesha ubora wao katika masomo ya sekondari.
Source: Florence Majani - MWANANCHI

No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA