AJALI YAUA TISA IRINGA NA WENGINE 61 WAJERUHIWA
WATU tisa wamefariki dunia na wengine 61 kujeruhiwa baada ya
basi walilokuwa wakisafiria mkoani Iringa, kupata hitilafu ya breki na
kutumbukia kwenye korongo.
Ajali hiyo ilitokea saa 8 mchana jana katika eneo la Mlima Ihemi, Wilaya ya Iringa
Vijijini, ikihusisha basi la abiria maarufu kwa jina la Usokomi Tours.
Basi hilo lilikuwa likitokea Iringa mjini kuelekea Kijiji
cha Usokomi wilayani Mufindi.
Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Iringa, Dk Faustine Gwanchele alithibitisha kutokea kwa vifo vya watu hao na
majeruhi na kuongeza kuwa, maiti
zimehifadhiwa katika chumba cha maiti cha hospitali hiyo.
Dk Gwachele alisema kuwa, alipokea maiti tisa, zote zikiwa
ni za wanawake ambapo sita zilitambuliwa.
Alisema kuwa, kati ya majeruhi 61 waliofikishwa hospitalini
hapo na kutibiwa, 33 waliruhusiwa huku 28 wakilazwa, baada ya hali zao
kuonekana zinahitaji matibabu zaidi.
Kwa mujibu wa mmoja wa askari polisi waliokuwa kwenye eneo
la tukio, ajali hiyo ilitokea baada ya dereva kuliegesha gari hilo wakati
wakiwa kwenye foleni wakisubiri kuruhusiwa wapite kutokana na barabara hiyo
kuwa kwenye ujenzi.
Alisema kuwa, dereva wa gari hilo alishuka akifikiri kondakta
wake ameweka kizuizi kwenye tairi, ili kulizuia lisirudi nyuma.
Askari polisi huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, kwa
kuwa siyo msemaji wa jeshi hilo alisema kwamba, wakati dereva huyo akiwa
ameshuka chini, ghafla lilianza kurudi nyuma.
“Ilibidi arukie na kwenda kukanyaga breki, lakini
ikashindikana na basi hilo likatumbukia kwenye korongo na kupinduka mara tatu,”
alisema askari huyo.
Alisema basi hilo lina uwezo wa kubeba abiria 64, lakini
inaelekea lilikuwa na idadi kubwa zaidi ya hao, wakiwa wamesongamana.
Mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo, Mchungaji John Mwakione,
ambaye alitibiwa na kuruhusiwa alizilaumu mamlaka za usimamizi barabarani kwa
kushindwa kuwa makini.
Desemba 3, ajali nyingine ilitokea eneo la Tanangozi mkoani humo na kusababisha vifo
vya watu watano, wanne
wakiwa wa familia moja .
Ajali hiyo ilitokea saa nane mchana wilayani Iringa katika kizuizi cha barabara ambapo unafanyika ukarabati wa Barabara Kuu ya Iringa - Mafinga mkoani Iringa.
Mashuhuda wa tukio
hilo walisema kwamba chanzo cha ajali
hiyo ni dereva wa gari dogo aina ya Rav 4 kuligonga kwa nyuma lori
lililokuwa na tela kwa nyuma, ikielezwa kuwa dereva wa gari hilo alikuwa
katika mwendo wa kasi ambapo alishindwa kulimudu, ndipo lilipoligonga lori
hilo.
Ajali hiyo ilipoteza maisha ya Ezekiel Mwaiteleke, mkewe,
watoto wake wawili na mfanyakazi wao waliokuwa wakitokea Dar es Salaam, kwenda
Kyela mkoani Mbeya,ambao walifariki
papohapo na maiti zote kupelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa.
Chanzo Cha Habari hii; MWANANCHI