WALIOKUWA MADIWANI WA CHADEMA JIJINI ARUSHA WAHUKUMIWA FAINI MAMILIONI.
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Arusha, imewaamuru waliokuwa
madiwani watano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jijini Arusha,
kulipa gharama zilizotumika kuendesha shauri lao lililotupwa na mahakama ya
mkoa kiasi cha sh milioni 15.1 kwa awamu mbili vinginevyo watapelekwa jela.
Aidha, kila mdaiwa aliamriwa kulipa sh milioni 3.2 ambapo
awamu ya kwanza ya sh milioni 1.51 walitakiwa kutoa mara baada ya uamuzi huo
kutolewa na kiasi kilichobaki wanatakiwa wawe wamelipa ndani ya kipindi cha
miezi miwili toka jana.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Charles
Magesa, mbele ya wakili wa CHADEMA, Method Kimomogoro ambaye pia alimtetea
Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe katika kesi ya awali ya
madiwani hao kupinga kuvuliwa uanachama.
Wajibu maombi katika shauri hilo waliokuwapo mahakamani hapo
wakati uamuzi huo ukitolewa ni Reuben Ngowi, Charles Mpanda na Rehema Mohamed,
huku wenzao, Estomii Mallah alitoa udhuru wa kufiwa na mwanaye na John Bayo
haikufahamika sababu za kutohudhuria.
Hakimu Magesa alisema kuwa, alifikia uamuzi huo baada ya
kusikiliza hoja za pande zote mbili ambapo alikubaliana na hoja za wakili
Kimomogoro aliyeieleza mahakama hiyo kuwa, wajibu maombi hao hawajaieleza
mahakama hiyo kama wana mali zinazoweza kukamatwa endapo watashindwa kulipa deni
hilo.
Alisema kuwa, alikubaliana na hoja za wakili huyo wa CHADEMA
kuwa wadaiwa hao hawajaionyesha mahakama kama hawana uwezo wa kulipa kwani
walikuwa wakiweka na kulipa wakili wa kutetea kwenye mashauri yote waliyokuwa
wakifungua sanjari na kulipia gharama mbalimbali za kesi.
Hakimu Magesa alisema kuwa wajibu maombi kupitia wakili
Lawena aliyekuwa akiwatetea kabla ya kujitoa, waliridhia kutoa viwango tofauti
vya fedha ambapo Mallah ni sh 20,000, Bayo sh 20,000, Mpanda sh 15,000, Rehema
sh 15,000 na Ngowi sh 25,000 ambaye tayari ameshalipa sh milioni moja.
Kwamba viwango hivyo ni vidogo na vitawachukua zaidi ya
miaka 10 kila mmoja kuweza kulipa kiasi cha zaidi ya sh milioni 3.02 anazopaswa
kulipa.
“Kimsingi madai haya yanatokana na kesi ya madai ambayo mtu
anayeifungua anajua kuwa endapo anashindwa kuna gharama atapaswa kuzilipa,
hivyo kutumia kipindi kirefu kulipa deni hilo mahakama haitaona kama yule
aliyeshinda kesi amepata matunda ya ushindi wake, kulipa deni hilo kwa miaka 16
ni kipindi kirefu mno na kitapoteza muda wa mahakama katika kufuatilia,”
alisema hakimu Magesa.
Hivyo akaagiza deni hilo lilipwe kwa mikupuo miwili huku
akiutaka upande wa waleta maombi kwenda gerezani kuleta mchanganuo wa gharama
za kumhudumia mfungwa ili kama wakishindwa kutekeleza amri hiyo ya mahakama
waweze kupelekwa huko.
Wakili kimomogoro alielezea kuridhishwa na uamuzi huo ambapo
alionyesha barua aliyopewa na mkuu wa gereza la mkoa wa Arusha ambapo
ilionyesha kuwa mfungwa mmoja hutumia kiasi cha sh 11,400 kwa siku kwa ajili ya
chai, chakula cha mchana na jioni, matunda na maji ya kunywa.
Kwa upande wao, madiwani hao waliotimuliwa CHADEMA
walielezea kuridhishwa na uamuzi wa mahakama ingawa walionesha masikitiko yao
dhidi uamuzi wa CHADEMA wa kuamua kuwadai fidia wakati hata wao walichangia
katika kukijenga chama hicho.
Agosti 10 mwaka jana, mahakama ya hakimu mkazi mkoa iliyokaa
chini ya hakimu Hawa Mguruta, ilitupilia mbali shauri la madai lililofunguliwa
na madiwani hao dhidi ya Mbowe na CHADEMA baada ya kubaini kuwa kulikuwa na
mapungufu ya kisheria.
Chanzo: Habari Leo
Chanzo: Habari Leo
No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA