UZINDUZI WA JIJI LA ARUSHA WAGHALIMU MILIONI124.
MADIWANI wa Chadema waliogoma kumtambua Meya wa Arusha,
Gaudence Lyimo sasa wanadaiwa kuanza kumtambua kupitia ‘mlango wa nyuma’.Tangu
ufanyike uchaguzi wa meya, kuliibuka mvutano wa kisiasa uliosababisha Chadema
kutangaza kutomtambua meya huyo.
Akizungumzia gharama za uzinduzi wa jiji juzi, Kaimu
Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Omari Mkombole alisema madiwani wa vyama vyote
walishiriki vikao muhimu vya kufanikisha sherehe hizo.
Itakumbukwa msimamo wa madiwani wa Chadema ni kutomtambua
meya huyo, huku wakisusia vikao kama ishara ya
kuonyesha msimamo wao.
Tayari, baadhi ya makada wa Chadema mjini hapa walitoa
msimamo wao kwa nyakati tofauti wakihojiwa kuhusiana na hali hiyo, huku
wakilaani kitendo hicho na kwamba kitendo hicho ni unafiki mkubwa.
“Taarifa
zilizonukuliwa nje kama ni siri zilikuwa ni makisio ya bajeti ambayo baada ya
kupitiwa ilibadilishwa na kupata bajeti halisi ya sherehe, siyo siri nyaraka
madiwani waliohudhuria wanazo, vikao vyote hivi vilifanyika kwa ushirikiano wa
madiwani wa TLP, Chadema wasiokuwa na mivutano na chama chao na CCM chini ya
Meya wa Jiji la Arusha,” alisema Mkombole.
Akichanganua fedha hizo, Mkombole alisema zilikuwa ni
Sh123,689,550, Mamlaka ya Maji safi
na Majitaka Arusha (Auwsa) walichangia Sh18,156,500 ambazo zilitumika
kukarabati mnara wa Azimio la Arusha.
Alisema Kampuni ya Jiangxi Geo Engeneering (Group)
Corporation inayojenga barabara za Jiji la Arusha ilichangia Sh12 milioni na China Railway
Seventh Group Co Ltd ilichangia Sh4
milioni.
“Halmashauri yenyewe imetumia Sh89,533,050 milioni
kugharamia sherehe hizo kwa shughuli mbalimbali zilizobakia, ikiwamo kuwalipa
wasanii mbalimbali walioalikwa, kugharamia chakula cha Rais, msafara wake na wageni waalikwa kwenye Hoteli ya Mt.
Meru,” alisema.
Mkombole alisema kamati iliyokuwa inasimamia chakula cha
Rais ilikuwa ikiongozwa na Efatha Nanyaro (Chadema), ambaye ni Diwani wa Kata
ya Levolosi akishirikiana na Paul Mathysen (CCM), Diwani wa Moshono.
Alisema ushiriki wa viongozi hao ambao ni wawakilishi wa
wananchi, unaonyesha suala hilo
lilifanyika kwa ridhaa ya Baraza la Madiwani kwa niaba ya wananchi.
Mwenyekiti wa madiwani wa Chadema, Isaya Doita alikiri
kushiriki hatua zote za maandalizi ya uzinduzi wa jiji hilo.
Source:Mwananchi

No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA