Asili Yetu Tanzania.Copyright
Happiness Magesse.
UPO msemo uliotawala vichwa vya watu tangu dahari kwamba wanawake ni
tabaka la kukaa nyumbani na kufanya kazi za ndani. Wao jukumu lao ni
kumfurahisha mume na lingine ni kuwaandaa watoto kwa ajili ya kwenda
shule na kufuatilia nyenendo zao darasani.Ilivyozoeleka ni kwamba
wanawake ni goigoi. Utaona bungeni kuna wabunge wa viti maalum ambavyo
wengi hutafsiri kuwa ni vya upendeleo. Kwa maana kwamba uwezo wao
kushindana kwenye majimbo na kushinda ni mdogo ndiyo maana wanapewa
hivyo maalum kwao.
Katika mitihani, kuna unafuu wa alama za ufaulu
kwa wanafunzi wa kike. Yaani wanaonekana hawana uwezo wa kushindana na
wavulana. Vijijini, wanawake wamekuwa wakitumika kama nyenzo ya kilimo,
yaani mama akalime ndiyo alishe familia, baba akacheze bao au kunywa
pombe.
Miaka inakwenda, wapo wanawake wengi ambao wameweza
kudhihirisha kwamba inawezekana kwa jinsi ya kike kuanzisha kazi na
kufanikiwa. Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk.
Asha-Rose Migiro ni mfano wenye nguvu kwa wanawake kufanikiwa.
Spika
wa Bunge, Anne Makinda, Mchungaji Getrude Rwakatare na wengineo, ni
kichocheo kinachotoa uthibitisho kuwa wanawake wanaweza. Ni suala la
kuwaamini na kuwapa nafasi, kwa hakika wanaweza kufanya mambo makubwa
mno.
Ukiachana na hao, ipo orodha ya wanawake vijana 10 ambao
wanastahili pongezi. Wamepambana katika maeneo yao kiasi cha kupata
mafanikio ambayo yameonesha njia. Inabidi tuwatambue na kuthamini
jitihada zao kwa maana wameendelea kuthibitisha ndivyo sivyo kwa wale
waliokuwa wanaamini kuwa wanawake si lolote kwenye utafutaji.
 |
| SUSAN MASHIBE |
Ni mwanamke jasiri, mpiganaji mwenye utaalam wa masuala ya anga
aliyethibitishwa na Mamlaka ya Anga Marekani (FAA). Anamiliki Kampuni ya
TanJet inayojihusisha na utoaji wa ushauri wa masuala ya anga ndani na
nje ya nchi.
Mwaka jana, alinukiwa Tuzo ya Kiongozi Kijana
Ulimwenguni (Global Young Leader), aliyopewa na Jukwaa la Uchumi Duniani
(WEF). Kampuni yake imekuwa ikipata tenda mbalimbali barani Afrika,
Ulaya, Marekani na kadhalika. Jopo la wajumbe wa Baraza la Congress
nchini Marekani, lilipotembelea Tanzania mwaka 2009, Mashibe ndiye
aliyeratibu masuala ya anga kuhusu ujio wao.
 |
| FLAVIANA MATATA |
Mwaka 2007 alipokwenda kushiriki mashindano ya dunia ya Miss Universe
na kushika nafasi ya sita, wengi walidhani huo ndiyo mwisho wake.
Ilionekana hivyo kwa sababu warembo wengi wameshiriki mashindano ya
dunia na baada ya kurudi nchini, hawakusikika tena.
Kwa Flaviana,
huo ulikuwa ni mwanzo wa kupiga hatua zaidi kusaka mafanikio yake. Hivi
sasa, mrembo huyo ni mwanamitindo wa kimataifa, anayefanya kazi na
makampuni makubwa ulimwenguni.
 |
| HAPPINESS MAGESSE |
Miss Tanzania aliyechukua taji hilo mwaka 2001, Happiness Magesse ndiye
aliyefanikiwa zaidi kimataifa kuliko wote, japo wapo wengine
wanaojitahidi. Hivi sasa Happiness ‘Millen’ ni mwanamitindo wa
kimataifa.
 |
| EMELDA MWAMANGA |
Ni mwanzilishi aliye pia Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Relim
Entertainment inayomiliki jarida maarufu la Kiingereza, Bang. Jinsi
alivyoweza kulisimamisha jarida hilo na kulifanya kuwa maarufu zaidi
nchini, inatosha kumpongeza kwamba ameonesha njia.
 |
| LADY JAYDEE |
Jina lake asilia ni Judith Wambura. Ni mwanamuziki wa kike mwenye
mafanikio zaidi ambayo chanzo chake ni muziki. Anamiliki bendi na
mgahawa wa kisasa ambao ulimgharimu zaidi ya shilingi milioni 100
kuuanzisha. Bila shaka Jaydee ameonesha njia kwa wanamuziki wengine wa
kike hapa nchini.
 |
| MADAM RITA |
Kuanzisha kitu wakati mwingine inaweza kuwa jambo rahisi lakini uimara
wa mtu ni pale anapoweza kulisimamia na kufanikiwa. Rita Paulsen
anastahili pongezi kwa namna alivyoweza kuanzisha Shindano la Bongo Star
Search na kulifikisha hapa lilipo. Huyu ni mwanamke kijana aliyeonesha
njia ya kweli ya mafanikio.
 |
| RAHMA AL-KHAROOS |
Anamiliki Kampuni ya RBP Oil & Industrial Technology. Uwezo wake
uliweza kuwashtua wengi pale alipoweza kujitolea mamilioni ya fedha
kuiwezesha Timu ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars. Mwanamke huyu ni
mfano tosha kwamba inawezekana kama tu utaamua kupambana.
 |
| SHEAR NASSA |
Anamiliki maduka ya Shear Illusions, vilevile ana jarida linaloitwa
Shear Hair & Beauty. Ukubwa wa maduka yake, heshima na umaarufu wake
kwa uuzaji wa vitu vya urembo ni kielelezo cha kumthibitisha Shear
kwamba ni mwanamke kijana aliyefanikiwa, kwa hiyo ameonesha njia.
 |
| KHADIJA MWANAMBOKA |
Mbunifu wa mavazi wa kike mwenye umaarufu kuliko wanawake wote nchini.
Ameanza harakati zake akiwa na umri mdogo na kwa alipofikia hivi sasa,
ameshaonesha njia kwa wanawake wengine nchini. Jambo muhimu ni kusimamia
fani yako mpaka kuifikisha kwenye kiwango bora. Khadija alipofikia kwa
ubunifu wa mavazi, anastahili pongezi.
 |
| FINA MANGO |
Alipata umaarufu mkubwa kwenye fani ya utangazaji wa redio lakini
alipoamua kuanzisha kampuni yake ya One Plus, ameweza kupata mafanikio
makubwa. Tenda ya kuratibu na kusimamia Tuzo za Muziki Tanzania (Tuzo za
Kili) kwa miaka mitatu mfululizo imedhihirisha ubora wa kampuni yake.
Imetolewa na Global publishers
No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA