WANAJESHI WAMTANDIKA ASKARI WA BARABARANI (TRAFIC) DAR ES SALAAM.
Asili Yetu Tanzania.Copyright
| Magari ya jeshi yakiwa yamezuiwa barabarani baada ya wanajeshi kumshambulia trafiki. (Picha na Mjengwa Blog) |
MWAKA 1979 Idd Amin anaishambulia Tanzania. Nyerere
anatangaza vita, wote tunakubali kupambana naye. Mimi na polisi wenzangu
tunapelekwa vitani tena mstari wa mbele. Huko tunakutana na wanajeshi, mgambo
na makundi mengine mbalimbali. Tumepambana mpaka mwisho. Tumeshiriki vita
Comoro, na nchi nyingine mbalimbali ambazo zilihitaji huduma za kijeshi. Huko
hakukuwa na cha Mwanajeshi au polisi, wote thamani yao ilikuwa sawa. Naenda
Darfur Sudan, huko nakuta polisi ana thamani kubwa tena analipwa vizuri kuliko Mwanajeshi.
Yaonekana UN wanajua thamani ya polisi katika jamii.
Leo narudi Tanzania
nakutana na kitu cha ajabu sana ambacho kinanifanya nishangae kweli kweli. Eti
Traffic Officer ambaye anaaminiwa kutawala makutano ya barabara ya Morogoro na
Mandela anapigwa makofi saa 10:15hrs asubuhi, mbele ya hadhara/kadamnasi ya
wapita njia, madereva na wafanyabiashara ndogondogo. Anayefanya hivyo ni
mwanajeshi. Ukitafuta sababu eti amewachelewesha wao watu muhimu wanaotoka
Mwenge kwenda kambini kwao Twalipo Temeke. Ni wakurugenzi wangapi wanasimama
barabarani kutii amri ya Traffic, ni mabalozi wangapi wanasimama barabarani
kufuata maelekezo ya Traffic, ni mara ngapi msafara wa Rais unashindwa kuanza
safari zake mpaka Traffic anapotoa taarifa kuwa barabara ni salama, ni mara
ngapi hata IGP anasimama barabarani kwenye foleni hadi aombe msaada wa
kupitishwa iwapo kuna dharura. Lakini leo mwanajeshi ambaye amepitia mafunzo ya
paredi tu, anamdhalilisha afisa wa polisi.
Niambieni wapiganaji wenzangu, katika jamii tunayoishi leo,
nani muhimu kati ya jeshi la polisi na Jeshi la Wananchi? Natoa masaa sita
wanajeshi wagome wasifanye kazi yoyote, walale nyumbani, kambi zao wafunge -
Je, kuna madhara gani kwa mwananchi, mwanakijiji wa kule Mtangimbole Songea, au
Nyantira kule Musoma? Baada ya wao kumaliza masaa yao sita, nawakaribisha
Polisi pia nao wagome kwa masaa sita - Wafunge vituo vyao vya polisi. Niambie
ni akina mama wangapi watabakwa, ni vibaka wangapi watavamia maduka na makazi
ya watu, ni benki ngapi hazitakuwa salama, msongamano wa magari utakuwaje, Je,
kuna mtu ataenda kazini, kuna uzalishaji mali utafanyika? Lakini hili haliwezi
kuonekana kwa leo, vinginevyo uwe na "Philosophical view".
Namkumbuka mbunge mmoja wa kaskazini ambaye ameomba
nisimtaje jina alipokuwa anachangia bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Yeye
alitoa angalizo kwa kusema, " Tabia ya kuweka tofauti katika maslahi kati
ya Wanajeshi na Polisi, kiasi cha wengine kulipwa mshahara mara mbili au tatu
ya ule wa mwenzake wa cheo kile kile, ni kukaribisha mgawanyiko wa wengine
kujiona bora kuliko wenzao". Haya ndiyo yale yaliyotokea jana pale Ubungo.
Mwanajeshi kwa kuwa analipwa tofauti, anamwona polisi sawa na mgambo.
Nimejisikia fedheha kwa sababu sio mara ya kwanza, au ya pili, au ya tatu.
Mwanajeshi kuvamia kituo kumchukua mwenzao ambaye ni mtuhumiwa si kitu cha
ajabu. Polisi tupo kimya. Hii dharau itaisha lini. Je, wanataka tufanye nini
ili tupate heshima tunayostahili?. Tugome; HAPANA, Tuvamie kambi za jeshi;
HAPANA, Tuondoe mahusiano yaliyopo kati yetu na wao; HAPANA, Nifanye nini sasa?
NA MOFIAS (Global Publishers)
No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA