TAASISI YA MASHEIKH NA WANAZUONI WA DINI YA KIISLAM TANZANIA, WATOA ONYO.
Asili Yetu Tanzania.Copyright
TAASISI ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislam Tanzania
imewaasa Watanzania kuzingatia utawala wa sheria na kutii amri za mamlaka
zilizoundwa kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam,
Katibu Mkuu wa Taasisi hiyo, Sheikh Khamis Mataka, alisema kuwa wamelazimika
kutoa kauli hiyo kutokana na baadhi ya Waislamu kuwa na ghadhabu na kusababisha
uharibifu wa mali za watu wasio na hatia na kuchoma makanisa.
Alisema taasisi hiyo ilifanya mkutano kwa siku mbili
kutafakari afya ya jamii kufuatia tukio la kunajisiwa kwa Kuran Tukufu na
ghasia zilizotokea Mbagala zilizohusisha kutotii sheria na amri za mamlaka na
uchomaji wa makanisa.
Sheikh Mataka aliongeza kuwa sekretarieti yao
imetazama suala la vurugu zilizotokea Kariakoo ambapo baadhi ya waumini
waliishia mikononi mwa vyombo vya dola na pia waliangalia vurugu za Zanzibar ndipo wakatoa tamko hilo.
Alisema taasisi hiyo imesikitishwa sana na baadhi ya Wasilamu kutumia
mikusanyiko isiyo halali kupingana na Jeshi la Polisi chini ya shinikizo la kutaka
kuachiwa watuhumiwa waliokuwa wamekamatwa.
Mataka alisema kinachofanyika sasa ni watu kutozingatia
mafundisho ya dini kwani yanahimiza utulivu, amani na kuheshimu kila
kilichowekwa kwa taratibu na kuwataka viongozi wote wanaohamasisha machafuko
kurejea mafunzo hayo kama msingi wa kudumisha
amani nchini.
Alibainisha kuwa taasisi hiyo imeshtushwa na baadhi ya
matamko ya viongozi wa dini ya Kikristo yanayotaka kuitumia kadhia hii kuutia
doa Uislamu na Waislamu na kujenga uhalali wa kuitikisa misingi ya udugu kiasi
cha kutamani kuzaliwa Tanzania
mpya.
Sheikh Mataka alisisitiza kuwa kauli ya maaskofu wa Kanisa
la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) iliyotolewa hivi karibuni ilikuwa na
mafumbo na hivyo kuzua hofu.
Hata hivyo alisema kuwa taasisi hiyo imesikitishwa na baadhi
ya askari waliotumia vibaya ruhusa ya kutumia nguvu katika kuzima fujo hizo,
bila kuzingatia mazingira na maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu na
shughuli za kiuchumi.
“Taasisi pia inatoa pole kwa Rais wa Zanzibar na Mkuu wa
Jeshi la Polisi kufuatia kuuawa kinyama kwa askari asiye na hatia, Saidi
Abdulrahman na pia kutokana na vurugu hizo tunatarajia kuitisha kikao cha
masheikh na viongozi wa taasisi mbalimbali za Kiislamu ili kutafuta dawa ya
tatizo hili,” alisema Mataka.
Aliongeza kuwa mbali na kuitisha kikao cha viongozi wa
Kiislamu lakini pia taasisi inatarajia kuitisha kikao cha viongozi wa dini
mbalimbali ili kujadili miundo bora ya kudumisha amani, utulivu na uhusiano
mwema baina ya wanadini kwa misingi ya kila mmoja kumheshimu mwenzake.
Taasisi hiyo pia iliwatahadharisha wanasiasa kujiepusha kwa
namna moja au nyingine kubariki vurugu za vikundi vya kidini na jamii kwa
ujumla na ikawataka waache kutoa ushawishi wa kujichukulia sheria mikononi na
kuhamasisha kutotii amri halali za mamlaka za nchi.
Akijibu swali la waandishi waliotaka kujua endapo angekutana
na Sheikh Ponda leo atamshauri nini, alisema atamwambia azingatie Uislamu
katika kufanya mambo yake.
Chanzo:Tanzania Daima
No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA