PEMBE ZA NDOVU KONTENA MBILI ZA DAIWA KUKAMATWA ZIKITOKEA TANZANIA NA KENYA.
Asili Yetu Tanzania.Copyright
![]() |
HABARI za maofisa wa forodha wa Hong Kong, nchini China
kukamata kontena mbili za pembe za ndovu zinazodaiwa kutokea Tanzania na
Kenya bila shaka zitakuwa zimewashtua na kuwakasirisha watu wengi hapa
nchini. Pembe hizo zenye thamani ya Sh5.4 bilioni zilikuwa na vipande
1,209 vyenye uzito wa tani nne na zilikamatwa nchini humo siku tatu
zilizopita zikiwa zimewekwa alama za kuonyesha kwamba zilikuwa zimebeba
plastiki chakavu na maharage aina ya roscoco.
Tukio
hilo linasemekana limewaacha midomo wazi maofisa hao wa forodha nchini
humo, kwani ni mara ya kwanza kwao kukamata kiasi kikubwa kama hicho
katika historia ya nchi hiyo. Kugundulika kwa pembe hizo kumeelezwa
kulitokana na taarifa zilizotolewa na maafisa wa Serikali ya China kwa
maofisa wa forodha wa Hong Kong kuhusiana na pembe hizo.
Ni
tukio ambalo pia limeishtua Serikali ya Tanzania, ambapo Waziri wa
Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki na Mkurugenzi wa Idara ya
Wanyamapori, Paul Sarakikya walishtuka kusikia kuwapo kwa tukio hilo la
kukamatwa kwa shehena kubwa ya pembe za ndovu kutoka Tanzania na Kenya
na kusema watachukua hatua kwa kusaidiana na Idara ya Polisi wa
Kimataifa (Interpol).
Habari zinasema Serikali ya
China imewakamata watu saba kuhusiana na pembe hizo. Tukio hilo bila
shaka ni pigo kubwa kwa Serikali ya Tanzania, ikiwa ni siku chache tangu
iombe upya kwa Umoja wa Mataifa kuuza akiba yake ya pembe za ndovu ili
kupata fedha za kuimarisha ulinzi, hivyo kumaliza kabisa tatizo la
ujangili. Ni tukio ambalo wachambuzi wa masuala ya wanyamapori wa
kimataifa wanasema linaweza kuinua mboni za mamlaka za jumuiya za
kimataifa na kujiuliza kama kweli Tanzania inayo dhamira ya kweli ya
kukomesha ujangili.
Tuliposema mwanzoni mwa tahariri
hii kwamba tukio hilo bila shaka litakuwa limewashtua na kuwakasirisha
watu wengi hapa nchini, tulikuwa na maana kwamba wapo baadhi ya
Watanzania ambao wamehusika kwa namna moja ama nyingine na biashara hiyo
haramu na kwa sababu wametanguliza ubinafsi na kuweka kando uzalendo,
wako tayari kuuza nchi yetu ili wapate utajiri. Kitendo cha kula njama
na raia wa kigeni kujenga mitandao ya kijangili katika mbuga zetu za
wanyama, hakiwezi kutafsiriwa vingine isipokuwa uhaini.
Tunapata
shida kuelewa kwa nini vitendo vya ujangili vimezidi kuongezeka. Pamoja
na kesi nyingi za aina hiyo kuripotiwa kupelekwa katika mahakama zetu
kila kukicha na polisi kudai wana ushahidi wa kutosha dhidi ya watu hao,
hivyo kuwafungulia mashtaka mahakamani, hatuoni matokeo ya kesi hizo.
Kutokana na uzito wa makosa hayo, wananchi wangetegemea kesi hizo za
uhaini na uhujumu uchumi siyo tu ziendeshwe kwa hati ya dharura, bali
pia usiwepo uwezekano wowote wa watuhumiwa kupewa dhamana.
Tunasema
hivyo kwa uchungu mkubwa kwa sababu tukio hilo la kukamatwa kwa vipande
1,209 vya pembe za ndovu zilizotoka Tanzania ni kubwa, kwani lina maana
kwamba vilitokana na kuuawa kwa tembo wasiopungua 500. Hiyo siyo idadi
ndogo kwa kipimo chochote kile na ni ishara kwamba Watanzania wamekosa
uzalendo kwa sababu haiwezekani ujangili mkubwa kiasi hicho ufanyike
pasipo kuwapo watu walioshuhudia na kuamua kukaa kimya.
Umefika
wakati sasa Serikali iache kutoa machozi ya mamba kila mara matukio
hayo yanapotokea. Lazima sasa vitendo vya ujangili vipewe adhabu kali
kama kifungo cha miaka 30 jela au hata kifungo cha maisha, mbali na
kuundwa kwa jeshi maalumu kama ilivyofanya Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar iliyounda KMKM kwa lengo la kudhibiti magendo ya karafuu.
Tatizo hapa ni kutokuwapo sheria kali zinazokwenda na wakati. Hivyo,
tusizilaumu mahakama kwa kutoa adhabu nyepesi kwa makosa mazito kwa
sababu mahakama hizo zinafanya hivyo kwa mujibu wa sheria zilizopo.
Chanzo cha habari hii ni MWANANCHI

No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA