Header Ads

Breaking News
recent

RAIS KIKWETE AKEMEA VITENDO VYA WANAOENEZA UDINI KATIKA JAMII.

Rais Jakaya Kikwete amewaonya baadhi ya wananchi wakiwemo wanasiasa na viongozi wa dini wanaoeneza udini katika jamii na siasa kuwa jambo hilo ni hatari kwa usalama wa nchi na amewataka waache mara moja kwani vinginevyo watawagawa watanzania na kuiingiza nchi katika machafuko na mauaji kwa agenda isiyokuwa ya watanzania.
 
Akiongea na viongozi wa ngazi mbalimbali za wilaya na mkoa wa Kagera na wananchi kwenye mkutano wa majumuisho ya ziara yake mkoani Kagera rais Kikwete amesema agenda ya udini inayoenezwa na watu mbalimbali siyo agenda ya Watanzania bali inaletwa na watu wenye nia mbaya wanaoionea wivu Tanzania kutokana na amani na utulivu ulioko nchini.
 
Rais Kikwete ametumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wa dini madhehebu yote wakristo na waislamu kuendelea kuwahubiria Watanzania kuhusu umuhimu wa amani, umoja na mshikamano na amesema ikiwa dini itaingizwa kwenye siasa, itafika wakati nchi itagawanywa kwa udini ambapo hata viongozi watachaguliwa kwa misingi ya dini jambo ambalo ni hatari na litaleta misukosuko na mifarakano katika jamii.
 
Aidha rais Kikwete amezungumza kwa uzito mkubwa kuhusu wahamiaji haramu ambao amesema lazima waondoke nchini kwani walipewa nafasi ya kuomba uraia lakini walioomba ni wachache na amesema tatizo hilo linaidhalilisha nchi kutokana na baadhi ya watendaji ikiwemo idara ya uhamiaji ambao wamekuwa ni sehemu ya tatizo kwa kushindwa kuchukua hatua kwa wakati.
 
Rais Kikwete amesema Tanzania siyo shamba la bili ambalo kila mtu anaweza kuingia na kufanya analotaka na kwamba tatizo hilo la wahamiaji haramu lisipodhibitiwa sasa litaleta matatizo makubwa ya mipaka na utawala katika wilaya zote za mkoa wa Kagera kwa miaka ijayo ambapo watanzania watakosa mahali pa kuishi ndaniya nchi yao kwani wageni watakuwa wengi zaidi na watakuwa na sauti kuliko wenyeji.
 
Chanzo Cha Habari: ITV TANZANIA

No comments:

KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA

Powered by Blogger.