WAZIRI AZINDUA USAFIRI WA NDEGE YA BEI NAFUU YA FASTJET
NAIBU Waziri wa Uchukuzi, Charles Tizeba ameagiza Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kuandaa mazingira mazuri na miundombinu
katika Viwanja vya Mwanza na Kilimanjaro kukabiliana na ongezeko la abiria
wanaotarajia kuvitumia.
Akizindua safari za ndege za Kampuni ya Fastjet Dar es
Salaam jana, Tizeba alisema kuanzishwa kwa safari za ndege za bei rahisi kwa
mikoa mitatu ya Dar es Salaam, Kilimanjaro na Mwanza kunatoa changamoto kwa
Serikali kuboresha miundombinu kukidhi mahitaji ya ongezeko la wasafiri.
“Kuanzishwa kwa safari za ndege za bei rahisi ya Sh32,000 na
Kampuni ya Fastjet kunatarajiwa kuvutia abiria wengi zaidi, hali ambayo viwanja
vingi nchini vikiwamo vya Mwanza na Kilimanjaro haviwezi kutimiza mahitaji,”
alisema Tizeba.
Tizeba alisema hadi sasa Serikali inaendelea kurekebisha
baadhi ya viwanja vya ndege nchini, vikiwamo vya Kigoma, Tabora na Mafia huku
Kiwanja cha Mwanza kikiendelea kurekebishwa sehemu ya abiria na barabara za
ndege.
“TAA ihakikishe hakuna abiria atakayeshindwa kusafiri kwa
sababu ya wingi wa watu na ukosefu wa miundombinu kwa kiwanja chochote cha
ndege nchini,” aliagiza Tizeba.
No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA