DEREVA WA PAROKO NA WENGINE SABA WANASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI KWA TUHUMA ZA UJAMBAZI WA PAROKO IRINGA.
IDADI ya watu wanaotuhumiwa kuhusika na ujambazi katika
matukio mawili tofauti kwenye Parokia za Kanisa Katoliki za Kihsesa na Isimani
mkoani Iringa imeongezeka na kufikia nane huku mmoja wa watu waliokamatwa akiwa
ni Dereva wa Paroko wa Parokia ya Isimani, Padri Angelo Burgio.
Tukio hilo ambalo lilisababisha mapadri wawili wa Parokia ya
Isimani ambao ni Paroko wa Kanisa hilo Padri Burgio na msaidizi wake Padri
Herman Myala na mlinzi wa Parokia ya Kihesa, Batholomeo Nzigilwa kujeruhiwa na
kulazwa katika hosptali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa lilitokea usiku wa Novemba
15 na 16 mwaka huu.
Akitaja orodha hiyo mpya huku akisisitiza kuwa msako wa
kuwatafuta watuhumiwa wengine unaendelea Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael
Kamuhanda alisema miongoni mwa watuhumiwa waliokamatwa ni pamoja na Dereva wa
Paroko huyo ambaye hivi karibuni ndiye aliyemsindikiza kwenda kuchukua fedha
Benki.
“Idadi ya watuhumiwa hadi sasa imefikia 8 na kati ya
watuhumiwa wanne waliokamtwa jana katika msako unaoendelea hivi sasa mmoja wao
ni Dereva Baba Paroko na ndiye aliyempeleka hivi karibuni kwenda Iringa Mjini
kuchukua fedha,” alisema Kamuhanda.
Wakati hayo yakiendelea, Serikali imesema vitendo vya
uvamizi wa Parokia za Kanisa Katoliki za mkoani Iringa hauna uhusino na
migogoro yoyote ya kidini inayoendelea nchini bali wahusika walifanya tendo hilo kwa tamaa ya
kujitatia utajiri wa haraka.
Akizungumza mara baada ya kutembelea mapadri waliojeruhiwa
kwa kwa risasi na mapanga wa Parokia ya Isimani mkoani Iringa Waziri wa Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu wa Mbunge William Lukuvi alisema Serikali imejipanga kukomesha vitendo
hivyo vya uhalifu hasa vinavyofanyika katika maeneo wanakoishi mapadri
wakigeni.
“Serikali itahakikisha inaimarisha ulinzi hususani katika
maeneo wanakoshi wamisionari kutokana na watu kujenga dhana kuwa kila anapoishi
mzungu huenda kuna fedha ama mali
wanazoweza kujipatia kwa nguvu kama
walivyowafanyia mapadre wa Isimani,” alisema Lukuvi.
Pia wazili Lukuvi alilitaka Jeshi la Polisi mkoani hapa
kutoa mafunzo maalumu kwa watu wanaofanya kazi za ulinzi kwenye nyumba zote za
misheni wanazoishi mapadri wawe na mbinu za kuwabaini kwa haraka majambazi na
kuwadhibiti kabla ya kusababisha
madhara.
"Hawa walinzi ambao wanalinda maeneo mbalimbali katika
misheni, taasisi na maeneo mengine wanatakiwa wapewe mafunzo ya ulinzi ili
amani iwe ya kuaminika katika maeneo hayo… jeshi la polisi kwa sasa wajipange
ili watoe mafunzo hayo kwa mfumo huo tunaweza kuzuia matukio ya wizi na watu kuvamiwa," alisema Lukuvi.
Naye Kaimu Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hosptali hiyo, Dk
Faustine Gwanchele alisema afya ya mapadri hao akiwemo Paroko Burgio
aliyefanyiwa upasuaji na kutolewa risasi tano mwilini inaendelea vizuri.
“Kwa sasa hali ya Padri Burgio inaendelea vizuri baada ya
kumfanyia upasuaji na kutoa risasi tano mwilini mwake, pia hali ya Padri
Hermani aliyecharangwa kwa mapanga inaendela vizuri isipokuwa mlinzi aliyepigwa
kichwani katika Parokia ya Kihesa, Botholomeo Nzigilwa hali yake ni mbaya na
tumempatia rufaa ya kwenda Muhimbili,” alisema Dk Gwanchele.
Akizungumzia tukio hilo
akiwa hospitalini alipolazwa Padri Myala (36) ambaye ni msaidizi wa Paroko wa
Parokio hiyo alisema majambazi walikuwa na mwenyeji kwani walionyesha wanajua
kila kona ya majengo ya Parokia hiyo.
Geofrey Nyang’oro na
Pius Kadinde Iringa
Source Mwananchi

No comments:
KARIBU UTOE MAONI YAKO HAPA